Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 14 Julai 2024, amezindua vihenge na maghala ya kisasa ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) mkoani Katavi.
Mradi huu mpya umeongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka mbalimbali kama mahindi, mtama, na mpunga katika Mkoa wa Katavi kutoka tani 5,000 hadi tani 28,000.
Maghala haya yana mfumo bora wa kupitisha hewa, unaoruhusu ufanisi katika uhudumiaji wa mazao kwa kutumia zana za kisasa kama matrekta, mizani, na lifti. Haya ni mafanikio makubwa yanayoonyesha dhamira thabiti ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza Sekta ya Kilimo nchini.