Morogoro. Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amempa wiki mbili Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Emmanuel Mkongo awe ametenga eneo na kujenga vibanda kwa ajili ya mama na baba lishe wanaotoa huduma nje ya stesheni ya treni ya kiasasa (SGR) ili waweze kufanya biashara katika mazingira safi, salama na yenye hadhi.
Malima amefikia uamuzi huo baada ya kutembelea stesheni hiyo Julai 12, 2024 na kukuta mama na baba lishe wakipanga vyakula chini, huku wateja wao wakiwemo abiria wanaosubiri treni wakila chakula wakiwa wamesimama.
Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa stesheni hiyo ni ya kisasa, hivyo huduma zote zinazotolewa katika stesheni lazima ziwe za kisasa tofauti na ilivyo sasa ambapo mama na baba lishe wamekuwa wakiuza vyakula kwenye eneo lisilokuwa rasmi na pia lisilokuwa na ubora.
“Hii ni treni ya kisasa, hapa wanakuja abiria kutoka maeneo mbalimbali na hata wa kigeni, Mkurugenzi hakikisha ndani ya wiki mbili hawa kina mama lishe na baba lishe wanatengenezewa mazingira bora ya kufanyia biashara zao nje ya stesheni hii, najua hilli halikushindi kwa sababu hujengi ghorofa, unatakiwa kujenga mabanda yenye ubora,” amesema Malima.
Awali, mama na baba lishe hao wamemuomba mkuu wa mkoa kuona namna atakavyowasaidia katika kukuza mitaji yao ambapo mkuu huyo wa mkoa amemtaka Ofisa Maendeleo wa Manispaa ya Morogoro, kukutana na mama na baba lishe hao kwa ajili ya kuwaelekeza namna ya kuunda vikundi vitakavyowafanya wapate mikopo.
Mmoja wa wanawake wanaouza matunda, Telesia Daud ameuomba uongozi wa Shirika la reli nchini (TRC), kuwatengea maeneo maalumu ya wafanyabiashara wa matunda nje ya stesheni hiyo.
Kwa upande wa madereva wa bodaboda na bajaji, Malima amewataka madereva hao kuwa waaminifu kwa abiria wanaowabeba ambapo pia amewatoa hofu kuwa Serikali ipo pamoja nao katika kuhakikisha wanatoa huduma bora na za kisasa.
Pia, Malima amewataka madereva hao wa bajaji na bodaboda kuwa nadhifu wakati wote na kuvaa vikoti vyenye namba na jina la kituo hicho cha SGR wanachoegesha.
Akieleza changamoto zinazowakabili katika utendaji kazi wao, mmoja wa madereva wa bodaboda, Emmanuel Jacob amesema ni pamoja kukosekana kwa choo nje ya stesheni hiyo ambacho wangeweza kukitumia badala ya ilivyo sasa ambapo wanalazimika kuingia ndani ya stesheni ama kujisaidia haja ndogo vichakani.
Jacob ametaja changamoto nyingine kuwa ni kukosekana kwa huduma ya maji ya bomba kwa ajili ya kunywa, hivyo ameuomba uongozi wa SGR kupitia kwa mkuu huyo wa mkoa kuwawekea tenki la maji.
Naye Athuman Hamisi, mjumbe wa chama cha wasafirishaji abiria kwa bajaji na bodaboda kijiwe cha stesheni ya SGR, amesema kijiwe hicho kina jumla ya bajaji zaidi ya 1,000, bodaboda 250 na teksi 50 ambapo wote wanatoa huduma ya kubeba abiria kutoka kwenye stesheni hiyo na kuwapeleka maeneo mengine ya mji wa Morogoro.
Amesema Julai 11, 2024, madereva wa bodaboda walifanya uchaguzi na kupata viongozi wao, hivyo amemtoa wasiwasi mkuu huyo wa mkoa kuwa abiria wanaopanda vyombo hivyo wako salama.
Akitoa taarifa ya utendaji kazi wa stesheni hiyo, mkuu wa kitengo cha habari na mawasiliano kutoka TRC, Jamila Mbarouk amesema hali ya usalama katika stesheni hiyo ni asilimia 100 kwa kuwa zimefungwa kamera za CCTV kwa ajili ya kuangalia abiria tangu anapoingia stesheni hadi anapopanda treni.
‘’Kamera hizo zimefungwa ndani ya treni kwa ajili ya kuangalia usalama wakati wote wa safari na pia wapo askari ambao wamekuwa wakipita kuona hali ya usalama wa abiria,’’ amesema.