Wakazi Dar hifadhini maji, kukosekana kwa saa 15

Dar es Salaam. Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) imetangaza kuwepo kwa ukosefu wa maji siku ya Jumanne, Julai 16, 2024 kwa muda wa saa 15 kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa 3 usiku.

Dawasa imetoa taarifa hiyo leo Jumapili, Julai 14, 2024 kwa wateja na wananchi wanaohudumiwa na mtambo wa kuzalisha maji Ruvu Juu.

Imetaja sababu ya katizo hilo la maji kuwa ni kuruhusu matengenezo kwenye bomba kuu la kusafirisha maji ghafi, kutoka Mtoni kwenda Mtamboni katika eneo la Mlandizi.

Dawasa imetaja maeneo yanayoathirika ni pamoja na Ruvu darajani, Ruvu JKT, Mlandizi, Mbwawa, Visiga, Mile 35, Misugusugu, Kongowe, Soga, Miembe Saba, Kwa Mfipa, Mwendapole, Tanita, Kwa Mathias, Kwa Mbonde, Picha ya Ndege na Lulanzi.

Maeneo mengine ni Kibaha, Kiluvya, Kibamba, Mbezi, Magari Saba, Mbezi Inn, Mshikamano, Mbezi, Kimara,Tabata, Kinyerezi, Kisukuru, Msigani, Maramba Mawili, Tabata, Kimara B, Kimara Korogwe, Bucha, Baruti, Ubungo, Ukonga, Pugu, Gongo la Mboto, Uwanja wa Ndege, Majumba sita , Kiwalani, Segerea, Kinyerezi na Kisarawe.

Juni mwaka huu katika maeneo mengi ya Dar es Salaam na Pwani, wakazi walikosa maji kwa saa 48 kuanzia Ijumaa Juni 21 hadi Juni 23, ambapo  Dawasa ilieleza sababu ya kukosa huduma hiyo.

Taarifa ya Dawasa ilieleza kuwa, hali hiyo ilitokana na kuwepo kwa matengenezo ya umeme kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwenye mitambo ya Ruvu Chini na Ruvu Juu tangu Jumamosi ya Juni 22, ambayo ilisababisha ukosefu wa huduma ya maji kwenye maeneo mengi ya Pwani na Dar es Salaam.

Ziara ya Waziri wa Maji, Jumaa Aweso aliyoifanya katika jiji la Dar es Salaam Juni mwaka huu, ilitokana na gazeti hili kuandika mfululizo wa ripoti maalumu kuhusu changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji, ikibainisha ukubwa wa tatizo kiasi cha kuwalazimu baadhi ya wananchi kutumia saruji kusafisha maji machafu wanayoyatumia.

Aweso alifanya ziara katika mkoa huo na kubaini kile alichokiita uzembe uliokuwa unafanywa na watendaji wa Dawasa.

Kutokana na mazingira hayo Juni 30 mwaka huu, Aweso alimsimamisha kazi Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Kiula Kingu na Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji wa Maji wa mamlaka hiyo, Shaban Mkwanywe.

Julai 3 mwaka huu Waziri Aweso alieleza kuwa katika  kukabiliana na ukubwa wa tatizo hilo, watafanya mambo mawili ikiwemo kuchukua hatua za dharura, ili wananchi wapate maji.

“Tumeanza kuchukua hatua za kinidhamu kwa watendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao. Tumeanza kutekeleza hilo kwa sababu ukicheka na nyegele anayetambaa kwenye magoti atakung’ata pabaya,” alisema Aweso.

Related Posts