Dar es Salaam. Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeitaka Manispaa ya Ubungo, kuzingatia maoni ya wafanyabiashara wadogo maarufu kama Machinga katika mpango wake wa kuliendeleza Soko la Simu2000.
Kauli hiyo ya CCM inajibu kile kilichoonekana kama hali ya kutoelewana kati ya Machinga na manispaa hiyo, baada ya kuamua kulikabidhi eneo hilo kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), kwa ajili ya kujenga karakana.
Julai 8, 2024, Machinga katika soko hilo walifunga maduka na kuweka vizuizi barabarani wakipinga uamuzi huo wa Manispaa ya Ubungo.
Lakini baadaye Julai 13, 2024, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alikutana na kuzungumza na wafanyabiashara hao, akiwaeleza kwa hatua iliyofikiwa mradi huo lazima utekelezwe.
Maelekezo hayo yametolewa leo Jumatatu, Julai 15, 2024 na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla wakati akijibu moja kati ya kero 42 alizozipokea kwa wananchi wa Wilaya ya Ubungo.
Kwa maoni yake, Makalla amesema wafanyabiashara hao wanapaswa kusikilizwa na utekelezaji wa mradi huo uzingatie maoni yao.
Ameshauri Mkuu wa Wilaya (Hassan Bomboko) na Mkoa (Chalamila), wanapaswa kusikiliza maoni ya wafanyabiashara na mradi utekelezwe kwa kuzingatia faida ya pande zote mbili.
“Yale mawazo waliyowapa mnatakiwa mkae pamoja, asubuhi nilimwambia Ndile (Mussa, kiongozi wa wafanyabiashara) kwamba nitaongea na mkuu wa mkoa,” amesema.
Hata hivyo, ameeleza anatambua Machinga hao walivyohamishwa kutoka barabarani na kupelekwa sokoni hapo.
Amesema kwa amani wafanyabiashara hao walihama kutoka barabarani na kwenda katika soko hilo
Pamoja na hilo, amewataka wakati mwingine wasiandamane badala yake wawatafute viongozi kukaa nao meza moja.
“Ukiniuliza niseme nitakwambia siku nyingine kuandamana sio suluhu, suala ni kukaa mezani kuzungumza,” amesema.
Akizungumza katika mkutano huo wa hadhara, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hassan Bomboko amesema pamoja na kero hiyo kabla ya kumalizika wiki hii atatatua kero zote zilizoibuka kwenye ziara ya Makalla.
“Hizi kero ndani ya wiki moja nitakuletea ripoti zitakuwa zimekwisha,” amesema Bomboko.