WALIMA zabibu, timu ya Dodoma Jiji, asubuhi ya leo Jumatatu iliwasili jijini Arusha kwa ajili ya kuweka kambi ya kujiandaa na msimu ujao wa 2024/25.
Ni mara ya pili kwa timu hiyo kuweka kambi Arusha tangu ilipopanda daraja kushiriki Ligi Kuu Bara msimu wa 2019/20. Mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 2022 ambapo ilikuwa inajiandaa na msimu wa 2022/23.
Timu hiyo ambayo msimu uliopita 2023/24 ilimaliza katika nafasi ya 12 ndani ya Ligi Kuu Bara kwa kukusanya pointi 33 baada ya mechi 30, imewasili ikiwa na maboresho mapya kuanzia benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha Mkuu, Mecky Maxime akisaidiwa na Nizar Khalfan, Peter Manyika ni kocha wa magolikipa na Francis Mkanula kocha wa viungo.
Pia wapo wachezaji wapya ambao wamesajiliwa na tayari wametambulishwa kama kipa Mkongomani, Allain Ngereza na mlinzi wa kulia, Dickson Mhilu wote kutoka Kagera Sugar.
Wapo pia nyota ambao wamesajiliwa lakini bado hawajambulishwa rasmi kama kiungo mshambuliaji ambaye ni Mkongomani, Jackson Mbombo na kiungo wa kati Emotan Cletus kutoka Nigeria wakitua hapo wakitokea Tabora United.
Maboresho hayo pia yameenda sambamba na kuongeza mkataba kwa baadhi ya nyota wake kama msambuliaji Yassin Mgaza, Fadhili Mwinyimvua, Emmanuel Martin na Zidane Sereri.
Wengine ni Augustino Nsata, Anderson Kimweri, Robinson Kamura, Mtenje Albano, Apollo Onyango, Mwana Kibuta na Mohamed Hussein.