Farid amkabidhi Chama namba 17, Mkude achukua 20

IMEFICHUKA kwamba, Mwamba wa Lusaka, Clatous Chama, msimu ujao atavaa jezi namba 17 ndani ya kikosi cha Yanga baada ya kutua katika timu hiyo akitokea Simba, huku Jonas Mkude naye akichukua namba 20.

Chama ambaye amejiunga na Yanga akiwa mchezaji huru baada ya mkataba wake na Simba kumalizika, amekabidhiwa jezi hiyo na Farid Mussa.

Taarifa kutoka ndani ya kambi ya Yanga iliyopo Avic Town, Kigamboni, Dar es Salaam, zimebainisha kwamba Chama amekabidhiwa jezi hiyo kutokana na kuomba baada ya kukuta ikiwa na mtu tayari.

Mtoa taarifa huyo amebainisha kwamba, Farid ambaye hivi karibuni aliongeza mkataba wa kuendelea kuitumikia Yanga hadi mwaka 2026, ameridhia kumpa Chama jezi yake huku yeye akichagua kuvaa namba 28.

Chama amekuwa akipenda kuitumikia jezi namba 17 ambapo huwa anaivaa ndani ya timu ya taifa ya Zambia na Simba alipokuwa anacheza kuanzia 2018 hadi 2024.

Wakati huohuo, Jonas Mkude ambaye msimu uliopita alitua Yanga akitokea Simba, msimu ujao naye ataonekana akiwa na jezi namba 20 badala ya 19.

Mkude alipotua Yanga alikuta jezi namba 20 inavaliwa na Zawadi Mauya, hivyo akalazimika kuchukua namba 19.

Baada ya hivi karibuni Mauya kuondoka kikosini hapo kutokana na mkataba wake kumalizika, ndipo Mkude fasta akachukua jezi hiyo anayoipenda zaidi ambayo amekuwa akiivaa tangu akiwa Simba zaidi ya misimu 10 aliyocheza hapo sambamba na timu ya taifa ya Tanzania.

Related Posts