TIMU ya Fountain Gate imekamilisha uhamisho wa aliyekuwa mshambuliaji nyota wa KVZ ya Zanzibar, Seleman Mwalimu ‘Gomez’.
Nyota huyo aliyewahi kuzichezea timu mbalimbali ikiwemo FGA Talents inayoshiriki Ligi ya Championship amejiunga na kikosi hicho kwa mkopo ili apate nafasi ya kucheza akitokea Singida Black Stars ambayo imemsajili kwa mkataba wa miaka mitatu.
“Ni kweli tumemtoa kwa mkopo kwa sababu bado ni mchezaji mdogo na anayehitaji muda zaidi wa kucheza ili kulinda kipaji chake, tuliangalia timu itakayompa nafasi ya kucheza na Fountain tukaona ni sehemu sahihi kwake,” kilisema chanzo hicho.
Akizungumza na Mwanaspoti, Gomez amesema kwa sasa ni mapema sana kuzungumzia timu atakayoichezea msimu ujao ingawa muda utakapofika mashabiki zake watafahamu, huku akiwaomba kumpatia sapoti kama ilivyokuwa pia msimu uliopita akiichezea KVZ.
Kwa upande wa Rais wa Fountain Gate, Japhet Makau alisema, watahakikisha wanaendelea kuboresha timu kwa kuingiza majina makubwa na yenye tija, wanayoamini yatakuwa na msaada mkubwa kwa msimu ujao wa mashindano mbalimbali hasa Ligi Kuu Bara.
Msimu uliopita Gomez akiwa na kikosi cha KVZ alionyesha uwezo mkubwa ambapo aliibuka mfungaji bora wa Ligi ya Zanzibar (ZPL), baada ya kufunga jumla ya mabao 20 na kuchangia mengine saba ‘Assisti’ katika michezo 27, kati ya 30, aliyocheza.