Jiji Dar kutumia Sh bilioni 10.7 kujenga barabara za ndani

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inatarajia kutumia Sh bilioni 10.7 za mapato ya ndani kujenga zaidi ya kilomita 6 za barabara kwa kiwango cha lami na zege.

Zabuni za ujenzi wa barabara hizo zilitangazwa katika mwaka wa fedha 2023/2024 na leo Julai 15,2024 jiji hilo limesaini mikataba na wakandarasi waliopewa kazi hizo.

Akizungumza wakati wa kusaini mikataba hiyo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mrisho Satura, amesema wamekuwa wakitenga asilima 10 ya mapato ya ndani kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kwa mujibu wa Satura, katika mwaka wa fedha 2022/2023 walikusanya Sh bilioni 81 lakini mwaka 2023/2024 wamekusanya Sh bilioni 111.7 ikiwa ni ongezeko la Sh bilioni 30.

“Tutaweka nguvu kubwa katika usimamizi wa mapato ili kuongeza ukusanyaji na kujenga barabara nyingi zaidi, tunawaomba wakandarasi muwe waadilifu fedha hizi ni za wananchi na zimetafutwa kwa jasho kubwa, mjisimamie wenyewe kazi zifanyike kwa kasi,” amesema Satura.

Amezitaja barabara hizo zitakazojengwa kwa mwaka mmoja ni Faru Mnyamani, Sukita, Mwanza, Dodoma, Udowe, Magengeni – Chang’ombe, African School – Sanene, Pugu – Majohe – Mbondole – Viwege, Kimanga – Mazda, Taliani, Masai Wawili, Soko la Kigogo, Pugu Kanisa Katoliki na Pugu – Majohe – Mbondole.

Barabara nyingine ni Kwa Mpalange – Mwanagati – Kitunda, Kiyombo – Kipera, Moshi, Titanic 1, titanic 2 pamoja na ujenzi wa box Kalavati Msumi – Bombambili, Kavesu – Liwiti, Kwa Mzava na Kisukuru.

Mkurugenzi huyo amesema pia miradi mingi ambayo haijatekelezwa kwa wakati ilisababishwa na kutokuwa na injinia mbobezi kwani aliyekuwepo alikuwa msanifu majengo daraja la kwanza hatua iliyowalazimu kuomba Tamisemi wabadilishiwe.

“Halmashauri ya Dar es Salaam ilifika wakati tunapoteza fedha mkandarasi analeta ‘certificate’ anasema amejenga hadi usawa wa linta analipwa, akija kupaua anaomba ten ana kipande ambacho kilishalipwa. Tuna ‘site’ za namna hiyo ambazo wakandarasi wamekimbia,” amesema Satura.

Amesema watahakikisha wanasimamia kikamilifu kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kuleta tija kwa wananchi.

Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto, amesema changamoto kubwa katika jiji hilo ni ya miundombinu na kuwataka wakandarasi waliopewa kazi hizo kufanya kazi kwa kasi.

“Ni aibu kuwapa kazi wakandarasi wa nje wakati wa ndani wapo, tumewapa wakandarasi wa ndani ili wazidi kukua kiuchumi hivyo, msituangushe, mfanye kazi kwa kasi na kwa weledi,” amesema Kumbilamoto.

Mwakilishi wa wakandarasi hao, Johnbosco Moshi, ameishukuru halmashauri hiyo kwa kuwaamini na kuahidi kufanya kazi kwa ufanisi na kuikamilisha kwa wakati.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala, Said Sidde, ameipongeza halmashauri hiyo kwa kutumia mapato ya ndani kuboresha miundombinu ya barabara na kuitaka kuendelea kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato ili kutengeneza barabara nyingi zaidi.

Related Posts