Maandalizi ya Olimpiki… Kambi ya Riadha usipime, yatafuna Sh23 milioni

MASHINDANO ya Olimpiki yatafanyika mwezi huu Paris Ufaransa huku Tanzania ikitarajiwa kuwakilishwa na wachezaji Sita wawili wakiwa ni wa mchezo wa kuongelea na wanne ni Riadha ambapo nyota hao watakuwa na kibarua kizito kuhakikisha wanafanya kweli na kurudi na medali.

Nyota hao kwa upande wa riadha ni Alphonce Simbu,Gabriel Geay,Jackline Sakilu na Magdalena Shauri ambao wote wanakimbia mbio ndefu Kilometa 42,ambapo wako chini ya kocha wa timu ya Taifa ,Antony Mwingereza na meneja Michael Washa.

Ikumbukwe kigezo cha kushiriki mashindano ya Olimpiki kwa mkimbiaji wa Marathoni upande wa wanaume ni masaa 2:08:10,Wanawake ni 2:26:50 ambapo Simbu alifuzu kupitia Shangai Marathon za China akitumia muda wa 2:05:39,huku Jackline Sakilu nae akifuzu kupitia mbio hizo kwa muda wa 2:26:50,mbio hizo zilifanyika Novemba 26,2023.

Magdalena yeye elipenya kupitia Berlin Marathon zilizofanyika Septemba 24,2023 akitumia 2:18:41 huku Geay akitokea Valencia Marathon ambazo zilitimua vumbi Disemba 2,2023 akitumia 2:04:33.

Kwa upande wa kuogelea ni Sophia Latif ambaye atashiriki mbio za mita 50,Collins Saliboko yeye atashiriki mita 100 zote za free syles ambapo wako chini ya kocha Alexander Mwaipasi.

Sasa wakati wengi wakiwa na matumaini makubwa na nyota hao kufanya vizuri kumbukumbu zinaonyesha kuwa imepita miaka 44 tangu Tanzania ipate medali mbili Olimpiki,medali pekee ambazo tuna dunda nazo hadi sasa.

Medali hizo za fedha zililetwa na Riadha kupitia nyota wake wawili enzi hizo wa mbio za viwanjani ambao walimaliza nafasi ya pili,Suleiman Nyambu mbio za Mita 5000 na nyingine ikichukuliwa na Filbert Bayi katika mbio za Mita 3000.

Mwanaspoti imetembelea kambi ya timu ya taifa ya Riadha ambayo ipo Sakina Jijini Arusha chini ya Shirikisho la Riadha Tanzania (RT).

Inaelezwa tangu timu ya taifa ya Riadha ianze kushiriki Olimpiki haijawahi kukaa kambi ya kishua kama ya mwaka huu,kambi hiyo imewekwa kwenye hoteli ambayo ina hadhi ya kimataifa,Medan hotel ambayo ipo Sakina Arusha mita 200 kutoka Barabara kuu ya Arusha-Namanga.

Ndani ya hoteli hiyo kuna vyumba na vyoo vya kisasa,lakini pia mtandao wa bure (free wife),ambayo inawapa nafasi wachezaji kuweza kuperuzi na kufatilia mambo ambayo yanaendelea duniani.

Pia kuna mazingira mazuri inayojumuisha sehemu ya kupumzikia pamoja na ulinzi wa kutosha.

Unaambiwa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT),imetoa nafasi kwa kila mwanariadha kuchagua aina ya chakula ambayo anataka lakini ambacho kinamfanya awe na nguvu hili kwenda kurudi na medali.

Ambapo wanariadha hao chakula ambacho wanakula inategemeana na mtu mwenyewe na vyote vinapatikana kambini hapo na mara nyingi ratiba ya mchana huwa ni ugali Samaki na usiku ni wali Kuku pia kuna kifungua kichwa kwa maana ya chai ya maana.

Kama ilivyo kawaida kwa timu zote ambazo zinaingia kambini posho huwa ni sehemu ya kutoa motisha kwa wachezaji lakini pia kutoa nafasi kwa kila mmoja kuwa na fedha ambayo inashika mfuko.

Sasa nyota hao wanakunja Sh50,000 kwa siku kutoka kwa RT ,ambapo pesa hiyo ilianza kutolewa Juni mosi mwaka huu kabla hata ya kuingia kambini.

Hili kuhakikisha wanamka bila migongo kuuma wala uchovu ambayo inawafanya kutimiza vyema majukumu yao wanariadha hao chumba ambacho wanalala gharama yake ni Sh60,000 kwa usiku mmoja.

Gharama za kambi hiyo kwa siku 28 ambazo wapo inatazamiwa kugharimu Sh23,520,000 ambapo inajumlisha posho, chakula na malazi kwa wanariadha hao wanne, kocha mmoja na meneja mmoja.

Ambapo Sh8,400,000 ni posho ya kila siku Sh50,000 pia Sh5,040,000 itakuwa ni gharama ya chakula kwa siku zote 28 na Sh10,080,000 ni kwa ajili ya malazi ambayo ni Sh60,000 kwa usiku mmoja hivyo kufanya jumla kuwa ni Sh23,520,000.

Kocha wa timu hiyo Antony Mwingereza anasema maandalizi yanaendelea vyema,vijana wako katika morali nzuri ya kuhakikisha wanakwenda kurudi na medali huku akifunguka ratiba nzima ya mazoezi ya vijana hao.

“Ratiba tunazifanya kwa vipindi vyote kwa maana ya mara mbili kwa siku  kuna wakati unaweza kwenda mbio za asubuhi (morning run),ukarudi ukanywa chai alafu ukaenda kutafuta kasi katika mashindano (speed work).

“Alafu jioni unaenda mazoezi ya kawaida ya kumalizia kwenye viungo yani mazoezi mepesi mepesi hivyo ratiba inategemeana na siku yenyewe”,

Anaongeza kuwa zipo siku ambazo wanaenda kasi ambayo sio kila siku ambapo pia wanapokwenda kutimisha ratiba siku ya jumamosi wanaenda mbio ndefu.

“Wiki nzima umefanya mazoezi unaenda kuijaribu kwenye jumamosi lakini pia inategemeana na kwamba mwalimu utakuwa umewapangia kwamba spidi ipi waende nayo”.

“Mara nyingine unapokwenda jumamosi kufanya mazoezi ni kipimo kwamba wanariadha wangu wamaendeleo gani katika mazoezi,wapi niongeze na wapi nipunguze”.

Anaongeza kuwa kwa sasa wametoka katika mazoezi ya kawaida ambapo wako katika mazoezi ya juu lakini wanapoelekea kwa maana ya siku ikikaribia itabidi ratiba ishuke ili kuwafanya wanariadha kutunza kile walichonacho.

Alphonce Simbu ni naodha wa timu hiyo anasema kambi ni nzuri na wanaendelea na mazoezi ambapo anaamini kwa namna ambavyo wamefanya maandalizi msimu huu anaona kabisa lazima watarudi na medali.

“Ukiwa katika kambi kama hii unakuwa katika hali ya utulivu,unajitenga na majukumu mengine hasa ya nyumbani,kikubwa unachokifanya ni mazoezi,mapumziko na kula unaenda mazoezi tena”.

“Kwa upande wake Jackline Sakilu aanaipongeza Shirikisho la Riadha Tanzania (RT),kwa mapinduzi makubwa ambayo wamefanya kuanzia kwenye maandalizi kwa ujumla ambayo kwao inawapa morali ya kwenda kufanya vizuri.

Rais wa RT,Silas Isangi anasema hili kuwafanya vijana kuweza kufanya kweli Olimpiki ni lazima uweze kuwaandalia mazingira mazuri wanapokaa lakini pia motisha ya kutosha.

Ambayo inawafanya wasiweze kuwaza vitu vingine badala yake inawafanya kuwaza ushindi na kurudi na medali kwani mikakati ni kwenda kushinda.

 “Tunaamini vijana wetu wanaenda kushinda na kurudi na medali ila niweke wazi kuwa riadha tunajivunia kuwa na mwendelezo mzuri wa kuwapeleka wanariadha Olimpiki”.

Isangi anaweka wazi kuwa wanatamani na wao kuona motisha kama ile ambayo imekuwa ikitoka kwa timu za Soka,Simba na Yanga zikiwa zinashiriki mashindano ya Kimataifa kwa maana ya motisha ya fedha ambayo imekuwa ikitolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan kwa kila goli linalofungwa.

“Na tunatamani labda bonasi kama ile iwekwe kwa hawa wanariadha wetu kwamba mkirudi na medali tutawapa kiasi kadhaa hii itaweza kuwafanya wakapambane sana”.

Related Posts