Majadiliano ya DPP, bosi wa Jatu  bado muafaka

Dar es Salaam.  Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya JATU PLC, Peter Gasaya(33), anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka mawili, likiwemo la kujipatia Sh5.1bilioni kwa udanganyifu, bado anaendelea na vikao vya majadiliano na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) ya kuimaliza kesi yake.

Gasaya anadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka Saccos ya JATU kwa madai kuwa fedha hizo atazipanda kwenye kilimo cha mazao, ili kuzalisha faida zaidi, wakati akijua kuwa ni uongo.

Wakili wa Serikali, Eva Kassa ameieleza hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Jumatatu Julai 15, 2024 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kujatwa, hivyo kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini alikubaliana na upande wa mashtaka na kuahirisha kesi  hadi Julai 29, 2024 kwa ajili ya kutajwa na kuangalia hatua waliyofikia katika majadiliano hayo.

Machi 12, 2024, Gusaya, alimuandikia barua DPP ya kukiri na kuomba apunguziwe adhabu dhidi ya mashtaka yanayomkabili.

Kutokana na barua hiyo, Mahakama ilitoa nafasi kwa Gusaya  kuanza majadiliano na DPP kwa lengo la kuimaliza kesi yake.

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kujipatia kiasi hicho cha fedha pamoja na kutakatisha Sh5.1bilioni katika kesi ya uhujumu uchumi namba 8/2023.

Katika shtaka la kwanza, mshtakiwa anadaiwa kati ya Januari mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 jijini Dar es Salaam, akiwa mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo, kwa udanganyifu alijipatia Sh5.1 bilioni kutoka Saccos ya JATU kwa kujipambanua kwamba fedha hiyo ataipanda kwenye kilimo cha mazao, jambo ambalo alijua sio kweli.

Shtaka la pili ni kutakatisha kiasi hicho cha fedha tukio analodaiwa kulitenda kati ya Januari mosi, 2020 na Desemba 31, 2021, jijini Dar es salaam.

Siku ya tukio na eneo hilo, mshtakiwa anadaiwa alijihusisha na muamala wa Sh5.1  bilioni kutoka katika akaunti ya JATU SACCOS iliyopo Benki ya NMB, tawi la Temeke kwenda katika akaunti ya JATU PLC iliyopo katika Benki ya NMB tawi la Temeke, wakati akijua fedha hizo zinatokana na kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Related Posts