Makandarasi wapewa siku 14 ujenzi barabara Dar

Dar es Salaam. Jiji la Dar es Salaam limewapa wakandarasi siku 14 za uangalizi katika ujenzi wa barabara na endapo watashindwa hawatasita kuvunja nao mkataba.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Julai 15, 2024 na Meya wa Jiji hilo, Omar Kumbilamoto katika hafla ya kusaini mikataba na wakandarasi watakaojenga barabara 20 zilizopo ndani ya jiji hilo kwa fedha za mapato ya halmashauri ambapo kati yake zipo za kiwango cha zege na kiwango cha lami.

Barabara hizo ni pamoja na Faru-Mnyamani, Sukita, Dodoma, Mwanza, Udowe, Magenge-Chang’ombe, African School, Sanene, Msumi-Bombambili, Kavesu na Liwiti.

Nyingine ni Kwa Mzava, Kisukuru, Pugu-Majohe –Mbondole – Viwege, Kimanga-Mazda, Talian, Masai Mawili, Soko la Kigogo, Pugu Kanisa Katoliki na Pugu Majohe.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kumbulamoto amesema Sh10.7 bilioni ni fedha za kodi zilizokusanywa kutoka kwa wananchi, hivyo ni lazima wananchi waone thamani ya fedha zao.

“Leo tuna furaha Baraza la Madiwani kutatua changamoto ya ubovu wa barabara kwa wananchi wake na hatutakuwa tayari kumfumbia macho mkandarasi anayefanya vibaya.

“Siku 14 tukikuangalia tukiona kazi haziendi tunaachana na wewe, tunataka kazi zifanyike usiku na mchana na tukiona unaenda vizuri tutaenda nawe katika awamu nyingine,” amesema Meya huyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema kilichofanywa na uongozi huo ni jambo la kupongeza, kwani sasa kelele za kuwa fedha zinazokusanywa na halmashauri zinaliwa zitapungua.

Awali, mkurugenzi wa jiji hilo, Jomaary Satura, amesema Sh10.7 bilioni za ujenzi huo wa barabara zilizotolewa ni kati ya Sh111.7 bilioni walizozikusanya katika mwaka wa fedha 2023/2024.

“Mapato hayo yameongezeka kutoka Sh81 bilioni ziliyokusanywa mwaka 2022/2023, ikiwa ni sawa na ongezeko la Sh31 bilioni ndani ya mwaka mmoja,” amesema Satura.

Katika ahadi yake, mkurugenzi huyo amesema wanatarajia kuongeza ukusanyaji mapato miaka ijayo, ili kuongeza ujenzi wa barabara nyingi zaidi hata kufikia za thamani ya Sh20 bilioni.

Akizungumza kwa niaba ya wakandarasi, Johnbosco Minja, amesema kinochowafanya wamalize miradi kwa wakati ni fedha, watu na mitambo na kueleza kwa mkataba walioingia na halmashauri hiyo hawaoni sababu itakayowafanya kushindwa kumaliza kwa wakati.

“Tunashukuru namna wakandarasi wazawa tunavyopewa kipaumbele na Serikali, niahidi tu kwamba hatutawaaungusha, tufanya kazi kwa ufanisi na kumaliza kwa wakati,” amesema mkandarasi huyo.

Related Posts