Mbowe akosoa mfumo wa elimu, auita wa kibaguzi

Dar/Arusha. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amekosoa mfumo wa elimu nchini akidai ni wa kibaguzi.

Amedai mfumo huo ni ishara kwamba Taifa linaenda kufa.

Mbowe amesema matabaka ya elimu yanazidi kukua,  kiasi kwamba Watanzania wenye fedha hukimbilia kuwasomesha watoto wao nje ya nchi.

Amedai hilo linatokana na Serikali kupuuza kujenga miundombinu ya elimu bora nchini.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Mashono, jijini Arusha ikiwa ni mwendelezo wa Operesheni ya +225 inayogusa mikoa minne ya Kanda ya Kaskazini, Mbowe amesema kutokana na tatizo hilo mwanafunzi anayemaliza elimu ya Tanzania hawezi kuwa na nguvu kwenye soko la ajira.

“Tumeanzisha matabaka ya elimu Arusha mnakumbuka miaka 20 iliyopita ulikuwa huwezi kuona gari ya njano imebeba wanafunzi.Tulikuwa hatuna ubaguzi wa elimu leo tuna ubaguzi wazazi wenye fedha wanasomesha watoto wao kwenye shule za lugha ya Kiingereza,” amesema,

Kwa mujibu wa Mbowe, tatizo hilo limenzia kwa kuwa marais, mawaziri na viongozi wengine, watoto wao hawasomi shule za kata kwa kuwa hazina vitendea kazi na walimu hakuna wa kutosha.

“Ni muhimu Watanzania tuvae ujasiri kupigania haki zetu, tunatoa kodi lazima tusimamie kuhakikisha fedha tunazotoa zifanye mambo yatakayotupa tija, ikiwemo kutuandalia kizazi kijacho chenye elimu bora na chenye ushindani,” amesema.

“Ukitaka kuua taifa,  ua uchumi, Taifa hili linakufa. Nchi yetu haifanyi maendeleo ya kutosha kwa sababu tunapuuza elimu ya watoto wetu na wazazi tumekubali elimu ya watoto wetu kuwa duni,” amedai Mbowe.

“Tunashangaa kwa nini wenzetu wa Kenya wanapiga hatua halafu Tanzania tuliopewa na Mungu kila kitu hatupigi hatua. Ni kwa sababu uelewa wa wananchi kuhusu haki zao msingi dhidi ya watawala haupo.

Amesema katika ziara amezunguka mipaka mingi, ukiwemo wa Namanga upande wa Tanzania na kubaini hakuna maji lakini upande wa Kenya wana majisafi na salama ndani ya nyumba.

Awali, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amesema kitendo cha Serikali kutenga kiasi cha Sh890 bilioni kwa ajili ya kununua magari mapya ya kutembelea viongozi, ni mwendelezo wa matumizi mabaya ya mali ya umma.

“Haiwezekani magari wawe wanabadilisha kila baada ya miaka miwili, wakati mimi nina gari aina ya Toyota Land Cruiser naitumia huu mwaka wa 20 sasa. Sh890 bilioni ni nyingi tungeweza kutengeneza viwanda 890 vyenye thamani ya Sh1 bilioni,” amesema.

Katika maelezo yake alitoa mfano kiwanda kimoja kingekuwa na uwezo wa kuajiri vijana 200, tatizo la ajira lingepungua nchini, huku akieleza fedha hizo zingepelekwa hata katika sekta nyingine badala ya kununua magari.

“Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kila mwaka inaonyesha ubadhirifu wa fedha za umma, lakini hakuna kiongozi anayewajibishwa ni jambo ambalo wananchi walipaswa kupinga,” amesema.

Lema amesema kuna wakati huwa anashangaa hasira za wananchi wa Arusha wanadiriki kuwachoma wezi moto, badala ya kuwadhibiti viongozi wanaotumia vibaya madaraka.

“Nimeshangaa sana kuna wakati ndugu zetu, wazazi wanakufa hospitalini kwa kukosa dawa, mtoto anaenda shule hakuna elimu nzuri, baba anaenda hospitali anagundulika na kansa anapoteza maisha. Huko kote hukusikia hasira unamchoma mtu aliyeiba kuku kwa sababu ya njaa,” amesema.

Amesema Tanzania inashindwa kupiga hatua na kufika mbali kwa sababu wananchi hawaiangalii kwa ukaribu Serikali kwa kudhibiti mianya ya wizi.

Kwa upande wake, Mbowe amesema bado dhamira za viongozi wa Tanzania siyo nzuri kwa sababu wanatumia fedha nyingi zinazotokana na kodi za Watanzania kwenye matumizi yasiyokuwa ya msingi.

“Tanzania kwa sasa inaendesha Ikulu tatu, gharama zote zinatokana na kodi za Watanzania. Waziri analipwa mshahara, posho analipiwa wafanyakazi wake, dereva, walinzi na mafuta ya gari,” amesema.

Amesema haiwezekani Serikali ikakopa fedha kuhamisha makao makuu Dar es Salaam lakini matokeo yake wanaacha nyumba Dar es Salaam na kwenda kujenga zingine Dodoma bila kujali hali ya maisha magumu wanayopitia wananchi.

“Ikifika siku ya Ijumaa wanapanda ndege, kodi ya Serikali wanakwenda Dar es Salaam. Jumatatu asubuhi wanapanda ndege nyingine wanarudi Dodoma, kodi za Watanzania hakuna anayehangaika,” amesema.

Mbowe amesema ukienda Dar es Salaam wizara zote zina majengo, hakuna watu na popo wamegeuza makazi yao kwa sababu tu makao makuu yamehamishiwa Dodoma.

“Gharama ya kuendesha Serikali kwa bajeti ya mwaka huu asilimia 51 ni kulipa madeni na asilimia 38 ni kulipa mishahara na posho na kuendesha Serikali na kilichobaki kwa maendeleo ya Watanzania hakifiki asilimia 10,” amesema.

Related Posts