Mganga wa kienyeji jela miaka 30 kwa kubaka mgonjwa wake

Morogoro. Mganga wa kienyeji, Selemani Hamza (39), mkazi wa Kijiji cha Katindiuka wilayani Kilombero Mkoa wa Morogoro amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumbaka binti wa miaka 16 aliyepelekewa ili amtibie.

Hukumu hiyo imetolewa leo  Jumatatu Julai 15, 2024 na Hakimu Samwel Obasi wa Mahakama ya Wilaya ya Kilombero, baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka ambao haukuacha shaka.

Mbali na kuhukumiwa hiyo,  Mahakama hiyo pia imemuamuru mganga huyo kumlipa fidia ya Sh500,000 binti huyo.

Awali, wakili wa Serikali, Dastan William  alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo Desembe 10, 2023.

Awali, ilidaiwa mahakamani hapo na wakili wa Serikali, Dastan William kuwa Desemba 10, 2023, mshtakiwa alimbaka binti huyo aliyekuwa amepelekwa kwake na baba yake, ili amtibu magonjwa yalikuwa yakimsumbua. Ilidaiwa alifanya  kosa hilo kwa makusudi, kwani alijua kufanya hivyo ni kosa la jinai.

Katika kesi hiyo namba 40266/2024,  upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi watano, akiwemo binti aliyebakwa pamoja na daktari aliyefanya vipimo vilivyothibitisha kuwa binti huyo amebakwa.

Related Posts