Mtuhumiwa wa mauaji ya wanawake 42 adakwa

Dar es Salaam. Polisi nchini Kenya wamethibitisha kumkamata mshukiwa wa mauaji ya kutisha na kutupa miili katika dampo la Kware eneo la Embkasi jijini Nairobi.

Mshukiwa huyo ametajwa kama mauaji anayepanga kuwaua watu na hajali uhai wa binadamu. Polisi imesema mshukiwa huyo amekiri kuwaua wanawake 42.

Mkurugenzi wa Uchunguzi Makosa ya Jinai, DCI Mohamed Amin leo Julai 15,2024 amesema wamemkamata mtuhumiwa aliyetambulika kwa jina la Collins Jumaisi Khalusa ambaye amekiri kuwaua wanawake 42 pamoja na mkewe, Imelda, kuanzia mwaka 2022 hadi Julai 11, 2024.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Nairobi, DCI Amin amesema, ”Tunashughulika na mtu mwenye shida ya akili aliyefanya mauaji mfululizo asiyeheshimu maisha ya watu”

Khalusa alikamatwa Jumatatu ya Julai 15, 2024 eneo la Kayole baada ya kufuatiliwa simu zake, ambapo DCI amebainisha kuwa kupitia muamala wa fedha alioufanya kwa kutumia nambari ya Josephine Owino ambaye pia alimuua ndio uliwasaidia maofisa uchunguzi kumfuatilia na kumtia nguvuni.

DCI amesema dakika chache kabla  mtuhumiwa hajakamatwa, alikuwa kwenye mpango wa kuendelea kumshawishi mtu mwingine ambaye alijulikana kama Susan kwa ajili ya kwenda kumtendea uhalifu.

“Mtuhumiwa alikuwa akimshawishi kwa nguvu mtu ambaye angekuwa mhanga wake wa baadaye, mwanamke aliyejulikana kama Susan, na maofisa wa uchunguzi wamemwita kutoa taarifa.”

Maofisa waliohusika kumkamata mhalifu huyo wamesema walikaa umbali wa mita 500 kutoka dampo la Kware eneo ambalo miili ya wanawake wanane ilipatikana kufikia Jumapili.

Kwa mujibu wa maofisa wa Polisi nchini Kenya, baada ya mtuhumiwa huyo kukamatwa aliwapeleka mpaka eneo alilotenda mauaji na DCI ameonyesha baadhi ya vifaa alivyokutwa navyo mtuhumiwa huyo ambaye inadaiwa  alivitumia kwa mauaji ikiwemo glovu, simu, mifuko na kitambulisho.

Kitu kingine ni panga ambalo polisi walidhani mtuhumiwa alitumia kutenda unyama pamoja na kamba.

Related Posts