Na Mwandishi wetu, Babati
MWENGE wa uhuru umezindua mradi wa maji wa mamlaka ya wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) uliopo kijiji cha Magara Halmashauri ya Wilaya ya Babati mkoani Manyara.
Meneja wa RUWASA wilayani Babati, Felix Mollel akizungumza kwenye uzinduzi wa mradi huo na mbio za mwenge amesema utahudumia watu 5,137.
Mhandisi Mollel amesema aina ya chanzo cha mradi huo maji ni mto Magara na mtandao una kilomita 20.7.
Amesema mkandarasi wa mradi huo ni kampuni ya Help desk engineering na chanzo cha fedha ni program ya P for R.
“Mradi umegharimu shilingi 801,748,043.24 na una vituo vya maji 18, valve 18 na chemba 16,” amesema mhandisi Mollel.
Mkuu wa wilaya ya Babati, Lazaro Twange, amesema mradi huo utawanufaisha wakazi wa kijiji cha Magara ambao wanaishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za mradi huo.
“Tunaukaribisha mwenge wa uhuru hapa Magara na endapo utaridhia utuzindulie mradi huu muhimu wa maji ambao utakuwa na manufaa makubwa kwa jamii,” amesema Twange.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kwa mwaka 2024, Geofrey Mnzava amewapongeza RUWASA kwa kukamilisha mradi huo ili dhana ya kumtua mama ndoo kichwani ikamilike na kuinufaisha jamii.
“Mwenge wa uhuru umeridhia kuzindua mradi huu wa maji wa kijiji cha Magara wenye thamani ya shilingi milioni 801 na kibao cha uzinduzi kipelekwe na kuwekwa kwenye chanzo cha maji,” amesema Mnzava.
Mkazi wa kijiji cha Magara, Hawa Juma amesema mradi huo wa RUWASA umekuwa mkombozi kwao kwani umesogeza huduma ya maji kwa karibu.
“Maji ni uhai na hivi sasa tunapata huduma hii kwa ukaribu tofauti na awali ambapo tulikuwa tunafuata mbali kule mton kwenda kuyachota na tunafurahia mwenge kutuzindulia,” amesema.
Pamoja na jumbe nyingine mwenge wa uhuru kwa mwaka 2024 una ujumbe wa “Tunza mazingira na shiriki uchaguzi wa serikali za mitaa kwa ujenzi wa Taifa endelevu”.