Dar es Salaam. Wakati matukio ya utapeli kwa njia ya simu yakiendelea kushamiri nchini, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ametoa ushuhuda wa jinsi alivyonusurika kutapeliwa, huku akionya vijana kuacha tabia hiyo.
Nape ametoa simulizi hiyo leo Jumatatu Julai 15, 2024 wakati akipokea taarifa ya hali ya mawasiliano mkoani Kigoma katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa.
“Hawa watu wanaotapeli mtandaoni si kwamba tu wanawaibia wananchi wa kawaida hata mimi nimeshatapeliwa nao, (bila kutaja kiasi alichotapeliwa) na hivi karibuni nikiwa bungeni kuna mmoja wa wabunge wenzangu aliomba nimchangie jambo fulani baada ya muda mchache nikapokea meseji kwenye simu yangu ikiniambia hiyo hela nitumie kwenye namba hii.
“Nilipoona ile meseji nikashtuka kidogo, mmmh.. imekuwaje baada ya muda mfupi kutoka kuzungumza na mheshimiwa mbunge natumiwa meseji hii, nilichofanya nami nikamuandikia meseji kuwa nimeshatuma Sh2.5 milioni akanitukana, nikajua alikuwa tapeli,”amesimulia Nape.
Simulizi ya Waziri Nape kuhusu uwapo wa utapeli kwa njia ya simu unapewa nguvu na ripoti ya robo mwaka unaoishia Machi 2024 ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inayoonyesha vitendo vya ulaghai kwa njia ya simu vimeongezeka kwa asilimia 43.
“Vitendo vya utapeli kwa njia ya simu Machi 2023 viliripotiwa 12,044 vimeongezeka hadi kufikia 17,245 Machi 2024,” imesema ripoti hiyo.
Ripoti ya TCRA, inautaja Mkoa wa Rukwa kuongeza kwa vitendo hivyo ukiwa umerekodi 6,861, ukifuatiwa na Morogoro (6,126) na Mbeya (1,625).
Aidha, katika ziara ya Waziri Nape mkoani Kigoma ambako anakagua minara iliyojengwa na kampuni mbili za mawasiliano nchini na Serikali ikichangia ruzuku ya zaidi ya Sh278.4 milioni, amewataka vijana kuachana na njia hizo za kujiingizia fedha.
“Vijana msishiriki vitendo vya utapeli, mtakamatwa tu kama wengine wanavyokamatwa maeneo mbalimbali nchini, licha ya kuwa vitendo hivyo bado vipo,”amesema Nape akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Kibondo mkoani humo.
Pia, amewataka vijana na watumiaji wengine wa mitandao ya kijamii kuitumia kujipatia maendeleo, kujenga umoja na mshikamano.
“Ndugu zangu Serikali inafanya uwekezaji mkubwa kwenye mawasiliano, nawaomba tuitumie kwa mambo mazuri, ikiwemo kukuza maendeleo yetu kiuchumi na kijamii, ili Rais wetu (Samia Suluhu Hassan) aendelee kuona manufaa ya uwekezaji huu ili azidi kutoa maelekezo na fedha nyingi zitumike kuimarisha mitandao ya mawaliliano nchini,”amesema Nape.
Aidha, Nape amewataka watumiaji wa mitandao ya kijamii kuacha tabia ya kuitumia kwa kutukana viongozi, kueneza vitu vya hovyo na vya uzushi.
Waziri Nape ameanza ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa minara 758 katika mikoa 26 ya Tanzania Bara ambayo itasaidia kutoa huduma ya maendeleo ya mawasiliano kwa wananchi zaidi ya milioni 8.5 wanaoishi vijijini ambapo ujenzi huo utakamilika 2025.