Siri ya PPRA kuibuka mshindi wa kwanza sekta ya udhibiti

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA), imesema ushindi walioupata kwenye maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabasaba unatokana na kufanya kazi kama timu na kutoa huduma bora kwa kuhudumia wateja zaidi ya 700.

Katika maonesho hayo mamlaka hiyo iliibuka mshindi wa kwanza katika kipengele cha mamlaka za uthibiti.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Eliakim Maswi, Meneja Kanda ya Pwani wa mamlaka hiyo, Vicky Mollel, amesema waliweka lengo la kuhudumia wateja 500 lakini walivuka hadi kuhudumia 700.

“Siri ya mafanikio ya PPRA ni kufanya kazi kwa pamoja kama timu na kujituma. Tulijipanga kutoa elimu ya matumizi ya Mfumo wa NeST kutokana na Sheria mpya ya manunuzi ya Umma.

“Tulitarajia ushindi kutokana na nguvu kubwa tuliyoiweka katika kuhamasisha umma na tulihakikisha banda letu linavutia wateja kupata huduma,” amesema Mollel.

Meneja huyo amesema tuzo hiyo itaongeza msukumo wa kutoa huduma kwa wateja na kujipanga kwa lengo la kuwafikia zaidi.

Amesema wanatamani maonesho yajayo ya waweze kuwahudumia wateja wengi zaidi ya 2000.

Aidha amewataka wadau, taasisi za umma na sekta binafsi kujiandaa kutumia Mfumo mpya wa NeST kwa ajili ya michakato ya ununuzi wa umma.

Amesema pia kupitia Sheria ya manunuzi ya Umma namba 10 ya mwaka 2023 kuna fursa nyingi na kuwataka Watanzania wajiandae kushiriki katika fursa hizo ili kukuza uchumi wa Tanzania.

Related Posts