TANESCO kuanza maboresho ya mfumo wa LUKU mikoa ya Dar na Pwani

Shirika la Umeme Tanzania TANESCO limetoa taarifa kwa wateja wake wote juu ya zoezi la maboresho ya mfumo wa Luku linatorajiwa kuanza Julai 22 mwaka huu kwenye mikoa ya Dar-es-salaam na pwani.

Maboresho hayo yanayolenga kuendana na viwango vya kimifumo vya mita za Luku vya kimataifa na kuongeza ufanisi na usalama wa mita nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa TANESCO Bi Irene Gowelle ameeleza  namna ya kufanya maboresho hayo na kusema ”

Kuanzia tarehe tajwa kwenye mikoa  husika iliyotangaziwa kuanza maboresho hayo , Mteja atakapofanya  manunuzi ya umeme kupitia risiti yake ya malipo au ujumbe wa simu atapokea makundi matatu yenye jumla ya tarakimu sitini (60)  kila kundi likiwa na tarakimu ishirini (20) ambapo makundi mawili ya mwanzo yatakuwa ni kwa ajili ya maboresho (Key change tokens)  na kundi moja la mwisho litakuwa ni umeme ambao utakuwa umenunuliwa na mteja”.

Mteja ataingiza makundi yote ya tarakimu kwa kufuata mpangilio kama utakavyokuwa unasomeka kwenye risiti ya malipo na kwa kubonyeza alama ya reli # au mshale wa kukubali kila baada ya kuingiza kundi moja na baada ya hapo mteja atakuwa amekamilisha kufanya maboresho na kuingiza umeme wake alionunua.

Ukomo wa maboresho haya utakuwa ni tarehe 24-11-2024.

Katika hatua nyingine amebainisha kuwa,  zipo changamoto ambazo wamezipata katika mikoa iliyoanza zoezi la maboresho ikiwemo uelewa wa namna ya kuingiza token za maboresho na baadhi ya mita kubainika kushindwa kupokea mabadiliko hayo.

Ameshauri iwapo mteja yoyote atapata changamoto hiyo apige simu kwa namba za huduma kwa wateja katika mikoa husika ambapo wataalamu wa TANESCO watakapofika na kubaini mita ina changamoto basi Shirika litawajibika kumbadilishia mteja huyo mita bure bila gharama yoyote.

Related Posts