Dar es Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Kanda ya Mashariki, limewataka watumiaji wa mfumo wa Lipa Umeme Kadiri Unavyotumia (Luku) kufanya maboresho yanayoendelea kwenye mfumo huo, ili kuendelea kupata huduma hiyo.
Maboresho hayo ambayo yataanza Julai 22 hadi Novemba 24, yanalenga kuendana na viwango vya mifumo ya Luku ya kimataifa na kuongeza ufanisi na usalama wa mita za luku nchini.
Akizungumza leo Jumatatu Julai 15, 2024, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa Tanesco, Irene Gowelle amesema Luku ambayo haitafanyiwa maboresho baada ya Novemba 24 haitaweza kuingizwa tokeni za umeme.
Irene ameeleza maboresho hayo yamefanyika katika mikoa mingine na sasa yanahamia Kanda ya Mashariki na kufikia Novemba 24, 2024 mikoa yote nchini itakuwa imefikiwa.
“Mteja atakaponunua umeme kwa mara ya kwanza kuanzia Julai 22 atapokea tarakimu kwenye makundi matatu, kila kundi likiwa na tarakimu 20. Kundi la kwanza na la pili la tarakimu litakuwa kwa ajili ya maboresho na kundi la tatu la tarakimu litakuwa la umeme utakaokuwa umenunuliwa,” amesema.
Ameongeza kuwa mteja atatakiwa kuingiza tarakimu zote katika kundi la kwanza na la pili, kisha kuingiza tarakimu za kundi la tatu litakuwa la uniti za umeme alionunua.
“Kazi hii ni bure na itafanyika mara moja tu kwa mteja, baada ya kufanya hivyo mteja atakuwa amefanya maboresho hayo na ataendelea kupata kundi la tarakimu ishirini kila anapofanya manunuzi ya umeme,” amesema Irene.
Wakati Tanesco ikitoa taarifa hiyo, watumiaji wamekuwa na maoni tofauti wakitaka elimu zaidi itolewe ili maboresho hayo yafanyike kwa usahihi.
Akizungumzia hilo, mkazi wa Tandika, Mariam Adam amesema ni muhimu ikatolewa elimu ya kina ili watumiaji wafuate maelekezo kukidhi maelekezo ya maboresho hayo.
“Nimesikia hilo tangazo, ila nafikiri kuna haja ya Tanesco kutoa elimu ya mara kwa mara, maana huku mitaani tupo watu wa viwango tofauti vya uelewa, isije ikafika hadi mwisho wa muda walioweka, halafu wengine wakawa bado hawajafanya hayo maboresho,” amesema Mariam.
Kwa upande wake, Gidion Mhilu amesema,” Hayo maboresho nimeyasikia, lakini hivi kwanini hao Tanesco wasifanye wenyewe kwa sababu Luku zote zipo kwenye mifumo yao si wangemaliza tu suala hili huko huko?” amehoji.