Arusha. Wakati takwimu za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), zikisema asilimia nane ya Watanzania wanakabiliwa na umasikini uliokithiri ikiwamo kukosa chakula, kupitia mpango wa kuwanusuru kaya masikini, mfuko huo umejizatiti kuwakomboa watu hao.
Katika takwimu hiyo ambayo ni karibu ya Watanzania milioni tano, Tasaf imesema lengo lake ni kuboresha maisha yao kwa kuwapa fedha, kisha kuwaingiza katika mfumo wa kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza kwenye kikao na waandishi wa habari pamoja na wahariri kikichofanyika leo Jumatatu Julai 15, 2024 jijini Arusha, Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf, Shedrack Mziray amesema ipo mipango wanayoitekeleza ili kuwakwamua Watanzania hao.
Wakati huohuo kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Tanzania ina watu milioni 61.
Mipango hiyo ukiwamo ule wa kukwamua kaya masikini unaokwenda hadi mwaka 2025 kaya zitakazokidhi vigezo zitafanyiwa tathmini kuwapisha wenzao.
“Asilimia nane ya Watanzania wote wana umasikini uliokithiri kwa maana hawawezi hata mlo mmoja kwa siku, pia kuna wengine asilimia 26 wenye umasikini wa mahitaji maalumu.
“Kwanza tunawaingiza kwenye daftari la kuwapa fedha ambayo inaanzia Sh24,000 kila baada ya miezi miwili lakini inatofautiana kila kaya, kisha tunawapa elimu na ushauri pamoja na kuwawezesha kijasiriamali kisha vikundi na kuwapa mitaji,” amesema.
Amesema hadi sasa kuna vikundi takribani 60,327 huku walengwa wakiwa 838, 241 ambao wananufaika, huku karibu Sh2 trilioni zikitumika kuwainua Watanzania hao.
Amesema kwenye mpango huo kuna watu wenye uwezo wa kufanya kazi na wale wasioweza kama wazee wenye umri mkubwa jambo linalowafanya wasiweze kutoka kwenye mpango.
Akifafanua kwanini wanawapa fedha watu hao, Mziray amesema kwa hatua waliyopo ya kushindwa kumudu milo mitatu kwa siku jambo lililopo ni kupewa fedha waweze kutoka katika hali ya chini kabisa kisha waanze kuzalisha kwa kuwezeshwa.
Akizungumza na Mwananchi, mmoja ya wanufaika wa Tasaf kutoka Kijiji cha Oldonyowasi kilichopo Halmashauri ya Arusha, Agness Sarakikye amesema alikuwa akishindwa kumudu mlo pamoja na familia yake.
“Kwa sasa tunapata milo miwili hadi mitatu na uwezo wa kununua sukari, watoto wanapata madaftari, kupitia Tasaf sasa nina mradi wa kuku nauza maisha yanaenda,” amesema.
Amesema alipoingia Tasaf alikiwa akipokea Sh36,000 kila baada ya miezi miwili ijapokuwa ni ngumu kukaa nayo miezi miwili lakini pamoja na familia yake wameweza kujibana.
Elizabeth Elifas, mkazi wa Oldonyowasi amesema alipojiunga Tasaf alikuwa akipokea Sh30,000 fedha ambayo amekuwa akiitumia kununua mahitaji ya mtoto wake shuleni pamoja na chakula
Ametaja vigezo vya kuwapata wanufaika wa Tasaf, Meneja Masijala ya Walengwa, Philippine Mmari amesema kuna vigezo vya kitaifa ikiwamo kaya zisizoweza kupata milo mitatu, hivyo zinashindia uji.
Amesema Tasaf inashirikiana na taasisi zingine za Serikali katika utekelezaji wa programu zake.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miradi Tasaf, John Steven amesema mpango huo umekuwa na awamu tatu zikijumuisha ukarabati wa miundombinu ya afya elimu na kuinua Watanzania kiuchumi.
Ametaja pia uwezeshaji kupitia ajira za muda, uchumi wa kaya, fedha kwa walengwa na ujasiriamali. Amesema hadi sasa kuna Watanzania zaidi ya milioni 5.2 wanawake wakiwa asilimia 55.7 huku wanaume wakiwa 44.3 wanaonufaika na mradi huo.
“Tunafanikisha haya kupitia, Serikali pamoja na mikopo na ufadhili wa wadau wa maendeleo ikiwemo Benki ya Dunia (WB), nchi wanachama zinazozalisha mafuta duniani OPEC+,” amesema Steven.