KIPA wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Juma Pondamali ‘Mensah’ yupo ukingoni kujiunga na Yanga Princess kama kocha wa makipa.
Nyota huyo wa zamani ambaye pia aliwahi kuwa kocha inaelezwa hadi sasa kuna uwezekano mkubwa msimu ujao akaitumikia timu hiyo katika eneo hilo kutokana na uzoefu wake.
Wakati huo huo Yanga Princess imetua kwa beki wa kati, Wema Richard aliyekuwa anakipiga Simba Queens msimu uliopita ikitaka saini ya mchezaji huyo.
Mchezaji huyo ambaye pia ana uwezo wa kucheza beki zote mbili anatajwa kwenda kuwa mbadala wa Wincate Kaari aliyetimkia Msimbazi.
BAADA ya kutambulisha wachezaji na benchi la ufundi, JKT Tanzania imehamia kwa mtathmini mchezo kwa njia ya video (video analyst), Faraji Muya ‘Enzo’.
Inaelezwa bado mazungumzo baina ya pande hizo mbili yanaendelea na kama kila kitu kitakwenda sawa atajiunga na JKT Tanzania kwa ajili ya msimu ujao.
FOUNTAIN Gate Princess imeanza kufuatilia kwa karibu saini ya beki wa kati anayehusishwa na Yanga, Anita Adongo.
Beki huyo alikuwa tayari amemalizana na Yanga Princess na kilichobaki ilikuwa kusaini mkataba mwezi ujao, lakini Fountain Gate Princess imeingilia kati.
KENGOLD inatajwa kuwania saini ya kiungo, Said Juma Makapu kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano. Kiungo huyo wa zamani wa Yanga amebakisha taratibu chache za kumalizia kwa ajili ya kusaini mkataba na klabu hiyo iliyopanda daraja msimu huu ikitokea Champioship.
BAADA ya watani wa jadi kufukuzia saini ya winga wa Alliance Girls, Mkenya Nelly Kache, hatimaye amekaa mguu sawa kuitumikia Yanga. Nje na Simba na Yanga, Fountain Gate Princess nayo ilikuwa miongoni mwa timu zilizokuwa zinahitaji huduma ya winga huyo aliyemaliza Ligi Kuu Wanawake msimu uliopita na mabao saba.
SIMBA Queens inaelezwa imemalizana na meneja wa zamani wa Fountain Gate Princess, Asia Jumanne aliyedumu kwa msimu mmoja katika kikosi cha timu hiyo. Inaelezwa kwamba mwanadada huyo tayari ameshasaini mkataba wa mwaka mmoja na kilichobaki ni kutambulishwa. Timu hiyo inapambana kujipanga zaidi kimataifa.