TRA yaendelea na utekelezaji maagizo ya Waziri Mkuu 

KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda amesema wanaendelea na utekelezaji wa maagizo yaliyowekwa na Serikali wakati wa kikao cha wadau cha kujadili na kutafuta suluhisho la mgogoro wa wafanyabiashara hasa wale wa kariakoo.

Amesema mpaka sasa wamekamilisha utengenezaji wa mifumo miwili ikiwemo wa kutoa nyaraka za manunuzi na wa bei elekezi eneo la forodha na kwamba mifumo hiyo ikianza hawatarajii kupata malalamiko kutoka kwa walipakodi.

Kamishna Mwenda amesema hayo leo Julai 15, 2024 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa TRA Makao Makuu Jijini Dar es Salaam.

Amesema, hatua hiyo ni utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwemo kusitisha kamatakamata na ufuatiliaji wa risiti za mashine za kielektoniki (EFD), kuongeza nguvu ya kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya kodi, kuweka mfumo wa utoaji nyaraka za manunuzi wakati wa uagizaji bidhaa, kubainisha na kusimamia orodha ya bidhaa nane kuwa na bei elekezi, kukamilisha maboresho ya mfumo wa Tancis na wataalamu wa forodha kukutana na Jumuiya za wafanyabiashara nchini ili kujadiliana taratibu za kiforodha,

Amesema TRA imejipanga kuongeza nguvu katika kutoa elimu kwa walipakodi na umma kupitia njia mbalimbali zikiwemo semina za mabadiliko ya sheria za kodi zinazogawa aina za walipakodi mfano Wauzaji wa Vitenge na wauzaji wa vito vya thamani.

“Mbali na semina Kuna Elimu ya mlango kwa mlango yenye lengo la kuelimisha na kutoa huduma kwa walipakodi wetu, kutumia mitandao ya kijamii kuelimisha, ikiwemo makundi ya WhatsApp ya wafanyabiashara kwa kutuma jumbe mbalimbali za kuelimisha kodi,kutumia matangazo ya magari na vipeperushi mbalimbali na vikao vya wadau ikiwemo washauri wa kodi wa Kariakoo na viongozi wa wafanyabiashara kwa kujumuisha Matangazo kwenye TV, Radio, Magazeti na kutumia wasanii au watu mashuhuri jambo hili litafanikiwa.

Amesema mfumo wa kuruhusu kutoa nyaraka za manunuzi umekamilika tangu Julai 3, mwaka huu hivyo wafungashaji bidhaa (consolidator) kila mfanyabiashara atapata taarifa za kiforodha pia ataweza kulipa kodi moja kwa moja bila kupitia kwa mfungashaji na kwamba ataelewa ni kodi gani imelipwa.

Amesema kukamilika kwa Mfumo huo kutasaidia kuhakikisha kila mfanyabiashara anapata nyaraka zake za kiforodha na pia ataweza kulipia kodi moja kwa moja bila ya kupitia kwa mfungashaji wa mizigo yaani (Consolidator).

Amesema, katika suala la Kubainisha na kusimamia vyema orodha ya bidhaa nane ambazo ni vitenge,Mashati,nguo nyingine,vipodozi,Vito vya thamani,nguo za ndani,leso na vesti zitawekewa bei elekezi kama ilivyo katika magari kazi hiyo tayari imeshafanyika na orodha ya bidhaa hizo nane tayari zimeshawekwa kwenye Tovuti ya TRA zikionyesha aina ya bidhaa, aina ya malighafi, vipimo vyake, bei ya bidhaa na kodi ya bidhaa husika.

Mwenda amesema maboresho ya TANCIS yakijumuisha mfumo wa Auto valuation yanaendelea na kwa sasa yapo kwenye hatua za utengenezaji wa mfumo na Maboresho hayo yatakamilika kufikia mwezi Januari, 2025 kama ilivyoelekezwa na Serikali.

“Mpaka sasa kampuni 16 za Wafungishaji mizigo (Consolidators) wanaoagiza bidhaa tayari wameshapewa mafunzo kwa ajili ya kuanza kutumia mfumo huo na zoezi hilo limeambatana na kutoa elimu na uwezo wa kutumia mfumo huo”.Amesema

Aidha Mwenda amesema TRA ilitekeleza agizo la taratibu za kiforodha hususani uthaminishaji na ugomboaji wa mizigo Julai3 mwaka huu kwani Kamishna wa Forodha aliitisha kikao cha majadiliano na viongozi wa Jumuiya za Wafanyabiashara Tanzania ambao waliwakirishwa na Viongozi wao 11.

“Katika kikao hicho, baadhi ya mambo yaliyojadiliwa ni pamoja na mfumo wa ufungishaji mizigo unavyofanya kazi na kujadili bei elekezi za bidhaa nane. Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendelea kutoa elimu kwa walipakodi na kufanya mapitio ya viwango vya kodi ili kuwawezesha wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari kulingana na thamani ya biashara zao ikiwa ni pamoja na kushughulikia changamoto zote za wafanyabaishara zilizowasilishwa Serikalini hususani zile ambazo hazihitaji mabadiliko ya sera au sheria,”Mwenda

Aliongeza:”katika kuboresha mahusiano na wafanyabiashara na kuhakikisha malalamiko yao yanashughulikiwa kikamilifu na hasa yale yanayohusu watumishi, hivi karibuni TRA itaanzisha mfumo wa kuwasilisha malalamiko yao ambayo yatamfikia Kamishna Mkuu moja kwa moja,”amesema.

Mwenda amesema kumekuwa na malalamiko kwamba kutokuwa na bei elekezi kwenye bidhaa za vitenge, mashati, nguo nyingine, vipodozi, Vito vya thamani, nguo za ndani, leso na vesti kunasababisha rushwa.

Pia amesema “Tunawafanyakazi wazuri sana wa mamlaka tutawajengea uwezo waweze kutoa huduma nzuri zaidi na wale wachache wasiowaadilifu tutachukua hatua bila kumuonea, tutawasikiliza kutafuta taarifa na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.”

Related Posts