Trump, anatarajiwa kuteuliwa na wajumbe wa chama wapatao 2500, pia kumtaja mgombea mwenza wake wa umakamu wa urais katika hafla hiyo ya jimboni Wisconsin nchini Marekani.
Kongamano hilo la siku nne, linakuja siku mbili tu baada ya kunusurikia kifo kwa kulengwa na risasi, tukio ambalo lilitokea katika mkutano wa hadhara wa kampeni. Mkasa huo ulimezusha hali ya wasiwasi katika maeneo yote nchini Marekani.
Ikiwa imesalia miezi michache kabla ya marudiano ya uchaguzi kati ya Trump na mgombea wa chama cha Democratic Joe Biden wa Novemba 5, kwenye mkutano wa kampeni wa Jumamosi wa huko Pennsylvania mshambuliaji aliweza kufyatua risasi kadhaa kwa uelekeo wa Trump, na kusababisha hofu kubwa kuzuka kwa wahudhuriaji.
Kuuwawa kwa mtuhumiwa wa jaribio la mauwaji
Katika mkasa huo Trump alijeruhiwa kwa risasi sikioni na baadae alionekana akivuja damu, huku vikosi vya kukabiliana na majanga ya moto walionekana wakiwahudumia watu wengine wawili waliojeruhiwa vibaya. Na kuwepo pia ripoti za mtu mmoja kufariki dunia,
Baadae maafisa wa Shirika la Ujasusi la Marekani FBI walisema muhalifu, aliuawa kwa kupigwa risasi na kikosi maalum na kulitaja jina lake kuwa Thomas Matthew Crooks aliyekuwa na umri wa miaka 20 kutoka Bethel Park, hukohuko Pennsylvania.
Shirika hilo lilisema mshambuliaji huyo hakuwa mtu waliyekuwa kwenye rekodi zao za watu wa mashaka na kuongeza kuwa uchunguzi watakaoufanya unatazamwa kama kitendo cha kigaidi cha nyumbani.
Biden: Mfumo wa kiusalama wa Republican uchunguzwe
Hata hivyo, wakati huu ambapo FBI ikiendelea na uchunguzi wa kutaka kufahamu ni kipo hasa kilichosababisha mashambulizi hayo, na kufuatia jaribio la mauaji, Rais Biden aliagiza vyombo vya usalama vya Marekani kuchunguza hatua za kiusalama za chama cha Reublican.
Soma zaidi:Biden ataka Wamarekani watulize joto la kisiasa
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Marekani kauli ya Biden kuhusu uchunguzi wa kiusalama inazusha mada yenye utata, ambayo inaweza kuwagawa wanachama wa Republican katika zoezi la upigaji kura, kama ilivyokuwa msimamo wa chama hicho katika suala la utoaji mimba na ile ya uvamizi wa bunge la Marekani, tukio la Januari 2021.
Vyanzo: DPA/AP/DW