Dar/Tanga. Wakati matukio ya watu kupotea na kutekwa yakiendelea kutikisa nchini, Jeshi la Polisi limekanusha kuhusika na matukio hayo na kuionya jamii kutotoa taarifa za uongo.
Taarifa ya Jeshi la Polisi imekuja ikiwa ni siku moja tangu, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, ACP Zacharia Bernard alipotoa taarifa kwa vyombo vya habari ya kumshikilia kada wa Chadema, Kombo Mbwana, aliyetoweka tangu Juni 15, 2024 na alikuwa akitafutwa na ndugu zake, hali iliyoibua hisia za kutekwa.
Tukio lingine la hivi karibuni ni la kutekwa kwa Edgar Mwakabela, maarufu Sativa tangu Juni 23, 2024, ambapo katika maelezo yake kwa vyombo vya habari, alidai alipotekwa Dar es Salaam kisha alipelekwa kituo cha Polisi Oysterbay na kuwekwa katika karakana ya kituo hicho na kusafirishwa kwenda Arusha na kisha akaenda kutupwa katika Hifadhi ya Taifa ya Katavi alikookotwa akiwa na majeraha.
Hata hivyo, akizungumza leo Julai 15,2024 mkoani Simiyu akiwa katika ziara ya kuzungumza na maofisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Camilius Wambura amesema jeshi hilo halihusiki na utekaji, bali limekuwa likiwaokoa wanaotekwa.
“Kwanza ifahamike kwamba hatuhusiki na shughuli kama hizo za utekaji wa watu, sisi ni jeshi linalolinda usalama wa watu na mali zao. Kwa hiyo wanaoleta tuhuma hizo ni vitendo vya utovu wa adabu, jambo hilo halikubaliki,” amesema.
Akitoa mifano, IGP Wambura ametaja tukio la kutekwa kwa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi na kuuawa mkoani Kagera, Asimwe Novath, akisema Jeshi la Polisi liliwakamata watuhumiwa, japo tayari mtoto alikutwa akiwa amefariki.
“Kuna mtoto mwingine alitekwa Geita na watekaji wakadai Sh5 milioni kwa wazazi wake. Jeshi la Polisi liliwakamata na kuokoa mtoto wao, wale watekaji ni Jeshi la Polisi?
“Kuna mtoto mwingine alitekwa Mbeya na kudaiwa wazazi wake watoe Sh20 milioni na mtoto alikuwa ameuzwa na mama yake kwa huyo mtekaji ili apate fedha kutoka kwa baba yao, hao ni Jeshi la Polisi?” amehoji.
Alisema kuna watu wanaojipoteza halafu wanadai wametekwa.
“Tumeshuhudia juzi Mwanza, mtoto mdogo wa miaka 12 amejiteka yeye na mdogo wake na kudai fedha, matendo mengi ya ajabu.”
“Jamii yetu ibadilike, iache matendo ya kihalifu, taarifa ya uongo, tuzingatie maadili,” amesema.
Wakati ndugu wa kada wa Chadema, Kombo Mbwana (29) wakinyimwa kumwona akiwa mahabusu leo, baadhi ya wanasheria wamekosoa hatua ya Jeshi la Polisi kumshikilia bila kumpeleka mahakamani.
Juzi Jumapili Julai 14, 2024 Kaimu Kamanda Bernard amesema mtuhumiwa huyo amekuwa akitumia vifaa vya kielektroniki pamoja na laini za simu za mitandao mbalimbali zisizo na usajili wake katika kutekeleza uhalifu huo kinyume cha sheria za nchi. Hata hivyo, hakueleza walimkamata lini.
Leo ndugu zake Mbwana akiwamo mama yake mzazi, Hellena Joseph walikwenda Kituo cha Polisi Chumbageni, lakini hawakuruhusiwa kumwona.
“Wenye simu ukiwauliza wanasema Kombo amepatikana Tanga wanasema kashikwa na Jeshi la Polisi, sikupata usingizi kwa kweli nikasema kesho asubuhi inabidi niende nikamuone mwanangu, siku zote hizi sipati raha nashinda hata na njaa nikimfikiria mwanangu,” amesema Hellen.
Kwa upande wake baba mzazi wa Kombo, Twaha Mbwana amesema alifika Tanga akiwa na shauku kubwa ya kumwona kijana wake, lakini ameishia kuambiwa kuwa anaumwa malaria bila kumwona.
“Tunasikia ana homa ya malaria hatupendi turudi bila kumuona lakini imetubidi turudi tukubaliane na masuala ya hapa tukubali yaishe ila naomba waendelee kumfanyia huo ustaarabu wanaomfanyia ili tuweze kumpata kijana wangu.”
“Tumefika Chumbageni leo asubuhi, tukaambiwa huyu bwana hajala chakula muda mrefu kamtafutieni kwanza,”amesema.
Amefafanua “tukaenda kumtafutia nikapata chai na kumpelekea, ila nikaambiwa anaumwa sasa sijui kinaendelea nini.”
Amesema anashukuru mtoto wake yupo hai lakini hajamuona bali anaomba kama imebainika ana kesi basi apelekwe mahakamani kwa ajili ya hatua nyingine zaidi.
Amesema walipouliza sababu ya kutomwona walielezwa kwamba watamwona kesho (leo). Alipotafutwa kwa ajili ya kulifafanua hilo, Kamanda Bernard alisema atafutwe jioni, lakini alipopigiwa tena hakupokea.
Akizungumza leo na Mwananchi, Mkurugenzi Mtendaji Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga amesema Ripoti ya Haki Jinai ilieleza matatizo makubwa ya Jeshi la Polisi ni kushikilia watuhumiwa kwa muda mrefu bila kuwafikisha mahakamani, au kukiri kuwa wanamshikilia mtuhumiwa husika.
“Haki ya Kombo iangaliwe, Jeshi la Polisi lijitathimini, bahati mbaya sana hatuna chombo cha juu sana kusimamia Jeshi la Polisi,” amesema.
Wakili Paul Kisabo wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), amesema kwa mujibu kifungu cha 32 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), mtu anapokamatwa na Polisi anapaswa kuachiwa kwa dhamana au kufikishwa mahakamani ndani ya saa 24.
“Akishikiliwa tofauti na hapo ni kinyume cha sheria na anaweza kufungua kesi mahakamani kuomba kuachiwa kwa dhamana au kupelekwa mahakamani kama zipo tuhuma zinazomkabili na anaweza kufungua kesi kudai fidia ya kushikiliwa kinyume cha sheria,” amesema.
Kisabo amesema Polisi wanapomshikilia mtuhumiwa wakili wake au familia yake inapaswa kutambua, ni kosa kukaa na mtuhumiwa bila kutoa taarifa.
Kuhusu aina ya ukamataji, Wakili Kisabo amesema Polisi anapofika kwa mtuhumiwa anapaswa kujitambulisha, kuonyesha kitambulisho na kueleza makosa ya kutaka kumkamata mtuhumiwa akiwepo kiongozi wa Serikali ya mtaa.
Akizungumza na Mwananchi, Kaimu Katibu wa Chadema Mkoa wa Tanga, Michael Haule amesema wameshawasiliana na mawakili wa chama hicho pamoja na wengine kutoka Sauti ya Tanzania, kwa ajili ya kuanza kufuatilia kesi hiyo itakapoanza.
Amesema mawakili hao watasaidiana katika kufuatilia kesi ya Kombo Mbwana atakapofikishwa mahakamani.
Haule amesema Kombo alitekwa tangu Juni 15 na na walitoa taarifa vituo vyote vya Polisi na walifika kwa Kamanda wa Polisi wa mkoa huo walikoelezwa hawana taarifa zake.
“Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Tanga alifika kwa Kamanda wa Polisi Tanga na kutoa taarifa na kuambiwa wanaifanyia kazi, Naibu Katibu Mkuu Chadema- Bara, Benson Kigaila naye tulikwenda naye kwa Kamanda wa Polisi wilaya wakakana, kiongozi wetu akawatuhumu kuwa wanahusika kumshikilia wakawa wakali,” amesema.
Amesema hata kupitia mikutano ya hadhara iliyofanyika mkoani Tanga, ambao Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alihutubia, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando alikuwepo na alielezwa suala la kutoweka kwa Kombo naye alisema Polisi wanafanya uchunguzi.
Haule amesema kwa nyakati tofauti walimfuata Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Handeni na kumueleza tukio hilo, lakini alikanusha jeshi hilo kumshikilia Kombo, huku akisisitiza upelelezi wa tukio hilo unafanyika na hata kupewa RB.
Kiongozi huyo wa Chadema alihoji wakati gani Kombo aliingia mikononi mwa Polisi kwani waliteseka kwa muda mrefu kumtafuta na walikana kumkamata.
Mwanaharakati kupitia mitandao ya kijamii, Martin Maranja kupitia mtandao wake wa X ameandika kuwa: “Tumemtafuta Kombo Mbwana Twaha vituo vyote vya Polisi Tanga. RPC na OCD wakasema hawajui alipo na kwa kuwa hawajamkamata na wao wanamtafuta. Kumbe wanamtafuta wamemficha.
“Tumekwenda hospitali zote, hayupo. Baada ya siku 29, Polisi wanasema wanamshikilia kwa makosa ya mtandao. Makosa ya mtandao kwa sheria zetu yana dhamana.”