Wafahamu wagombea wawili wanaochuana na Kagame – DW – 15.07.2024

Mgombea wa kwanza ni Frank Habineza, anayewakilisha chama cha Democratic Green Party (DGPR), alipata asilimia 0.48 pekee ya kura mwaka 2017 na kuwa mmoja wa wanasiasa wawili wa chama hicho bungeni.

Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 47 ni mwanachama wa zamani wa chama tawala cha Kagame cha Rwandan Patriotic Front (RPF), lakini alikihama mwaka 2009.

Alikimbilia Sweden mwaka 2010 baada ya kifo cha makamu wa rais wa chama chake ambacho hakikutatuliwa, lakini mwaka 2012 aliahidi kurejea Rwanda ili kuimarisha demokrasia nchini humo.

Rwanda I Mgombea urais Frank Habineza
Frank Habineza wa chama cha kijani akiwa kwenye moja ya mikutano yake ya kampeni. Picha: Guillem Sartorio/AFP/Getty Images

Wakati wa kampeni zake, Habineza, amesisitiza kuongezwa kwa mishahara ya madaktari na walimu, kukomeshwa kwa kodi za makazi na kupendekeza kilimo cha kisasa kwa kuzingatia kulinda mazingira.

Aidha, mgombea huyo amekuwa akishinikiza uhuru zaidi wa kujieleza, huku akichukua tahadhari ya kutomkosoa moja kwa moja Kagame, ambaye amekuwa mtawala mkuu wa Rwanda tangu kumalizika kwa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 ambayo yaligharimu maisha ya watu 800,000, wengi wao wakiwa Watutsi.

Habineza, amepuuzilia mbali shutuma kwamba kugombea kwake ni njia ya kuwaridhisha wafadhili wa nchi za Magharibi.

Mpayimana, mgombea binafsi anayetumai kutoa upinzani dhidi ya Paul Kagame 

Mgombea urais nchini Rwanda, Philippe Mpayimana
Mgombea urais nchini Rwanda, Philippe Mpayimana.Picha: Eric Murinzi/AP Photo/picture alliance

Mgombea wa pili katika kinyanganyiro cha urais nchini Rwanda ni Philippe Mpayimana ambaye sasa anahudumu kama mtaalam mkuu katika Wizara ya Umoja wa Kitaifa na Ushirikiano wa Kiraia. Katika uchaguzi uliopita alipata asilimia 0.73 tu ya kura katika jaribio lake la mwaka 2017.

Mwanahabari huyo wa zamani aliondoka Rwanda na kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwaka 1994, katika wakati ambao mamia ya maelfu ya Wahutu walikimbia harakati za wanamgambo wa Kagame wengi wao wakiwa Watutsi, katika siku za mwisho za mauaji ya kimbari.

Mpayimana mwenye umri wa miaka 54 aliishi Ufaransa mwaka 2003, baada ya kukaa Kongo-Brazzaville na Cameroon, na tangu 2012 amekuwa akiishi katika mataifa hayo kwa muda pamoja na Rwanda.

Akizungumza na shirika la habari la AFP, Mpayimana amesema anajiona kama “mpinzani wa amani” ambaye anagombea urais “bila kuonyesha uadui wowote”.

Miongoni mwa ajenda zake katika kinyangayiro cha urais wa Rwanda, anataka kurekebisha Kanuni za Kazi, kukarabati na kuendeleza miundombinu ya usafiri.

Related Posts