Unguja. Wananchi zaidi ya 400 katika Kijiji cha Paje Mkoa wa Kusini Unguja, wameingiwa wasiwasi kuhusu kuhamishwa eneo hilo, kupisha ujenzi wa uwanja wa ndege wakidai hawajashirikishwa.
Wasiwasi huo unatokana na kuwapo mpango wa Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kutaka kujenga uwanja wa ndege katika eneo hilo.
Wamesema wamekuwa wakiona wataalamu wanaenda kupima maeneo yao lakini hawana taarifa yoyote wala kushirikishwa.
Mkazi wa eneo hilo, Haji Nuru Said amesema wao hawapingani na mipango ya Serikali, lakini wanachotaka ni ushirikishwaji ili watambue iwapo wakihamishwa wapi wanakwenda au vinginevyo.
“Kuna utata unaojitokeza watu wanakuja kupima kwenye maeneo yetu lakini hatuna taarifa na hatushirikishwi, tunaomba mchakato wote tushirikishwe na kujua kinachoendela,” amesema.
Kauli hiyo imeungwa mkono na Abubakar Mtumwa anayesema: “Sisi hatupingi maendeleo lakini tunasikia huko tu hatushirikishwi kwenye hatua zote ili kuridhia au kama tutatakiwa kuondoka tujue ni wapi tunakwenda na katika misingi gani.”
Hata hivyo, Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dk Khalid Salum Mohamed amewataka wananchi hao walio karibu na eneo hilo linalotarajiwa kujengwa uwanja wa ndege, kuondoa wasiwasi kwani Serikali haiwezi kufanya uamuzi bila kuwashirikisha wananchi wa eneo husika.
Dk Khalid amesema bado mchakato huo upo kwenye hatua za awali, kwa hiyo iwapo kukiwa na uamuzi wa kujenga uwanja huo, lazima wananchi watashirikishwa na ikiwezekana hata watakaotakiwa kupisha watalipwa fidia.
“Serikali haiwezi kufanya jambo bila kuwashirikisha na hakuna mwananchi atakayeondolewa kwenye eneo lake. Kinachofanyika kwa sasa bado ni upembuzi yakinifu iwapo uamuzi ukifikiwa kila kitu kitakuwa sawa,” amesema Dk Khalid.
Kwa sasa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ina mipango ya kujenga viwanja vya ndege katika maeneo ya utalii ili kurahisisha ufikaji.
Miongoni mwa maeneo hayo ni Paje Mkoa wa Kusini Unguja na Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.