Mbeya. Wavuvi, wafanyabiashara na wananchi waliopo pembezoni mwa Ziwa Nyasa katika mwalo wa Kafyofyo wilayani Kyela mkoani hapa wameonyesha hofu ya kupata magonjwa ya mlipuko kufuatia kukosa vyoo na kujikuta wakijisaidia kando na ndani ya ziwa hilo.
Watu zaidi ya 3,000 wanafanya shughuli zao pembezoni mwa mwalo huo, awali walikuwa wakitumia choo kimoja chenye matundu sita kilichosombwa na maji.
Hivyo kwa sasa kila mmoja anamaliza haja zake anapoona panafaa, hali inayohatarisha afya zao.
Katibu wa mwalo huo, Said Mwamambi amesema iwapo itatokea mlipuko wa magonjwa, hakuna mvuvi atakayebaki salama kutokana na kujisaidia vichakani, mchangani na wengine ziwani.
Amesema licha ya kwamba walishakuwa na choo, lakini tangu kiliposombwa na maji hawana sehemu ya kujistiri na kuiomba halmashauri kulifanyia kazi.
Naye Peter Mwamtima ambaye ni mfanyabiashara katika mwalo huo amesema licha ya kulipa ushuru lakini hakuna huduma muhimu katika eneo hilo, akieleza kuwa Serikali inawakamua tu bila kutoa huduma.
“Ukiikamua ng’ombe maziwa lazima uipe majani, sasa Serikali inachofanya ni kutoza ushuru tu haitoi huduma, choo imekuwa changamoto hapa tunaomba huduma hii” amesema Mwamtima.
Kwa upande wake Oscar Mwamakula ambaye ni mvuvi amesema mwalo huo unakusanya zaidi ya wavuvi 3,000 akieleza kuwa changamoto ya choo imekuwa kero, hivyo zinahitajika juhudi za haraka kuepusha athari kwa wananchi.
“Huu mwalo una wavuvi na wafanyabiashara zaidi ya 3,000 wanalipa ushuru lakini miundombinu hakuna, hii inatupa wakati mgumu sana katika majukumu yetu” amesema Mwamakula.
Naye mtoza ushuru katika mwalo huo, Tangulini Mwambopo amesema anakutana na changamoto kubwa katika kukusanya ushuru kutokana na wavuvi na wafanyabiashara kulalamikia matumizi ya tozo hiyo.
“Wanalalamika wakihoji matumizi ya ushuru hawaoni faida yake kwa kuwa miundombinu si mizuri kuanzia barabara hadi maeneo mengine, wanadai pesa inaenda halmashauri” amesema Mwambopo.
Diwani wa Kata ya Kajunjumele, Elia Mwandima ameliambia Mwananchi leo Julai 15, 2024 kuwa kwa sasa ni ngumu kujenga vyoo eneo hilo kutokana na kujaa maji akieleza kuwa wanapambana kukarabati kilichopo chenye matundu 12.
Amesema kulikuwapo na vyoo vingine vilivyojengwa na forodha, lakini viliharibika na iwapo hakutakuwapo namna nyingine watalazimika kufunga shughuli katika mwalo huo.
Akizungumza kwa njia ya simu, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Florah Angelo amesema kufungwa eneo hilo bado ni mapema akieleza kuwa mkakati wao ni kurekebisha miundombinu hiyo.
“Siyo kwamba vyoo hakuna isipokuwa vilivyopo vimejaa maji, hivyo tunapambana kuvikarabati viwe kwa juu, maji yapite chini kwa sasa mazingira ya pale yamejaa maji hakuna namna ya kujengwa vipya hadi maji yatakapokauka” amesema Mkurugenzi huyo.