ACHENI TABIA ZA KUJITEKA NA KUSINGIZIA POLISI  – IGP WAMBURA – MWANAHARAKATI MZALENDO

 

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Camillus Wambura kwa mara ya kwanza amezungumzia taarifa zinazolihusisha Jeshi la Polisi kuhusika katika matukio ya utekaji wa watu mbalimbali hapa nchini, akibainisha kuwa jeshi hilo halihusiki na matukio hayo.

IGP Wambura ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa Habari, mara baada ya kuweka jiwe la Msingi jengo la Mkuu wa Polisi Bariadi Mkoani humo pamoja na kuzungumza na Askari wa Jeshi hilo katika kituo kikuu cha Polisi Bariadi.

Wambura amebainisha kuwa Jeshi hilo haliwezi kuhusika na matukio hayo, ambao ameeleza katika baadhi ya matukio wamebaini kuwa watu wamekuwa wakijiteka kisha kutoa taarifa za uongo kuwa wametekwa.

“Haya matukio ya watu kutekwa au kupotea yamezungumzwa sana na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Mambo ya ndani, niseme hapa Jeshi la polisi halihusiki hata kidogo na matukio haya, na wale wote ambao wamekuwa wakitutuhumu wanatukosea heshima na adabu,” amesema IGP Wambura.

Mkuu huyo wa Polisi nchini, amewataka wananchi kuacha tabia za ajabu za kujiteka kisha kulisingizia jeshi la polisi kuhusika katika matukio hayo na badala yake wabadilike kwa kuacha kutoa taarifa za uongo.

 

Related Posts