Baraza la wadhamini Yanga matatani

Dar es Salaam. Yanga imepokea hukumu ya kutotambulika kwa Baraza la Wadhamini la klabu hiyo kufuatia hukumu iliyotolewa Agosti 2, 2023 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

 Hukumu hiyo ambayo Mwananchi imeipata nakala yake inatokana na kesi ya msingi iliyofunguliwa Agosti 4, 2022 na walalamikaji Juma Ally na Geoffrey Mwaipopo, wakitaka kutotambulika kwa Baraza la wadhamini la Yanga lililowekwa madarakani kwa katiba ya mwaka 2010, kukosa sifa kisheria.

Aidha, walalamikaji pia walitaka miamala yote ya fedha iliyoidhinishwa na baraza hilo, kutotambulika kisheria kwa kuwa ni batili.

Hukumu hiyo, imeitaka bodi iliyokuwa madarakani kwa katiba ya mwaka 1968 iliyofanyiwa mabadiliko mwaka 2011, kurudi madarakani kuongoza klabu ya Yanga.

Inaelezwa walalamikaji walirudi mahakamani kukazia hukumu hiyo kuiondoa madarakani bodi hiyo wadhamini ndipo uongozi wa Sasa wa Yanga ukapenyezewa taarifa.

 Baraza linalolamikiwa linaongozwa na Mwenyekiti George Mkuchika na wajumbe wake Mama Fatma Karume, Dk Mwigulu Nchemba, Tarimba Abbas na Antony Mavunde.

Ingawa viongozi wa juu wa Yanga hawakupatikana kufafanua hukumu hiyo lakini Mkurugenzi wa Sheria wa Yanga, Wakili Simon Patrick amekiri klabu yao kupokea taarifa hiyo.

Simon, amesema Yanga inafuatilia hukumu hiyo ambayo tangu kufunguliwa kwa kesi hiyo klabu yao haikuwa inajua lolote kabla ya Sasa kupokea wito wa kuitwa mahakamani.

“Nikweli Kuna hiyo hukumu lakini niseme kuanzia kufunguliwa kwa kesi hiyo, Yanga haikuwa na taarifa yoyote na hata hukumu ilipotoka pia hatukuwa tunafahamu,”amesema Patrick.

“Tumechukua hata jitihada za kuwatafuta hao walalamikaji kama ni wanachama wa klabu yetu, hatuoni taarifa zao kwenye orodha ya wanachama wetu halali wa klabu,” aliongeza kusema wakili huyo.

“Kama tungefahamu tungechukua hatua za hata kuitetea klabu lakini kwa sasa tunafanya juhudi za kujua undani wake na ikiwezekana kwa kuwa walalamikaji wamerudi mahakamani kukazia hukumu na sisi tutaangalia nafasi ya kukata rufaa kwa kuwa klabu haikuwa inafahamu lolote na Ina haki ya kusikilizwa.

Endelea kufuatilia Mwananchi.

Related Posts