Njombe. Mhudumu wa grocery ya kuuza vinywaji Faraja Bembela (28), mkazi wa Kijiji cha Lusisi kilichopo wilayani Wanging’ombe ameuawa kwa kunyongwa na mtu anayedaiwa kuwa ni bosi wake (jina limehifadhiwa) kwa madai ya kusababisha hasara ya Sh50,000.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga hayo amesemwa hayo leo Jumanne Julai 16, 2024 wakati akizungumza na Mwananchi Digital kwa njia ya simu, huku akisema bosi huyo amekimbia na wanaendelea kumtafuta.
Amesema marehemu ameuawa kwa kushambuliwa sehemu mbalimbali za mwili wake na kunyongwa kwa kushirikiana na kijana mwingine ambaye amekamatwa.
Kamanda Banga amesema marehemu alianza kushambuliwa akiwa ndani ya grocery hiyo lakini baada ya kuona wamemuua wakamchukua na kwenda kumtupa katika Misitu ya Tanwatt iliyopo wilayani humo.
Amesema tukio hilo limetokea Julai 14, 2024 saa kumi alfajiri chanzo kikitajwa kuwa ni mahesabu wakati wa kukabidhiana na bosi wake kulionekana kuna hasara ya Sh50,000.
“Jambo hilo lilisababisha bosi kushikwa na hasira na kuanza kumshambulia, kwa hiyo tunaendelea na uchunguzi mara tutakapokamilisha huyu mtuhumiwa tuliyemkamata tutamfikisha mahakamani wakati tunaendelea kumtafuta huyu mtuhumiwa mwingine ambaye ametoroka na ndiyo muhusika halisi bosi wa huyu marehemu,” amesema Banga.
Amesema taarifa ya marehemu huyo kuuawa iligundulika baada ya kuona siku iliyofuata mpaka kufikia mchana grocery hiyo haijafunguliwa ndipo baadhi ya watu waliokuwepo kwenye tukio kueleza marehemu walimuacha na mtuhumiwa aliyekamatwa pamoja huyo bosi.
Kamanda Banga amesema baada ya kuonyeshwa mwili huo wa marehemu ulikutwa ukiwa umechomwa moto baadhi ya viungo na shingo kuvunjwa na kunyongwa kulingana na maelezo ya daktari.
Hata hivyo, amesema wamiliki wa grocery mkoani Njombe watakaokiuka sheria kwa kukesha wakiuza vinywaji kinyume cha utaratibu uliowekwa watachukuliwa hatua za kisheria.
Ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwa kuwa akisema Sh50,000 wangeweza kukubaliana na kukatana kwenye mshahara.