Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ni kama amekiomba radhi Chama cha Mapinduzi (CCM) kuhusu kauli yake ya kuwataka wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo kuacha kuandamana kwenda katika chama hicho, badala yake waende ofisi yake.
Akifafanua Chalamila amesema dhamira ya kauli yake kwa wafanyabiashara hao ni kuwataka wangeandamana kwenda ofisi za chama hicho ngazi ya wilaya badala ya Taifa kama walivyofanya.
Kwa mujibu wa Chalamila, kilichofanywa na wafanyabiashara hao Julai 11, mwaka huu ni kama kumchongea kwa viongozi wa juu wa CCM, akieleza asingependa kuikosa nafasi aliyonayo sasa.
Julai 12, alipozungumza na wafanyabiashara wa soko la Kariakoo, Chalamika alisema: “Mlichokifanya wafanyabiashara kwenda CCM jana ni sawa na mgonjwa wa malaria kwenda mtu asiyetibu malaria. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ipo mlipaswa kuja hapa kwa kuwa ndiyo tunaolisimamia na sio huko mlikokwenda.”
Ufafanuzi wa Chalamila umetolewa siku moja tangu, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla aeleze wafanyabiashara hao walikuwa sahihi kwenda ofisi za chama hicho.
Katika kauli hiyo, Makalla amesema kwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan alishawaelekeza viongozi wa chama hicho na Serikali kupokea kero za wananchi, hakuna namna CCM inaweza kujitenga nao, hivyo walichofanya ni sahihi kwenda katika chama hicho.
Chalamila ametoa ufafanuzi huo leo Jumanne Julai 16, 2024 alipozungumza kwenye mkutano wa hadhara katika ziara ya Makalla ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam.
“Mheshimiwa Makalla, wafanyabiashara kwenda makao makuu ya CCM ni kupotea njia kwa sababu ni kama wamekwenda kunishitaki, nilimaanisha wangeenda hata ofisi ya wilaya, mkoa na hata ngazi za chini kabla ya kufika makao makuu,” amesema.
Kwa kuwa wameamua kuvuka ngazi mbalimbali, amesema ameona ajitetee kwa kuwaeleza walipaswa kwenda ngazi za chini kabla ya kufika juu.
Amesema msingi wa kuyafafanua hayo ni kuondoa kile alichokiita minong’ono inayoendelea katika mitandao ya kijamii kwamba yeye siyo mwanaCCM.
“Naomba niseme hapa Wazo (Kawe) mimi ni mwanachama wa CCM nisiyetiliwa shaka, nafahamu ofisi ndogo ya Lumumba ndipo anapopatikana Mwenyekiti wa CCM (Rais Samia).
“Hatua ya wafanyabiashara kwenda pale ni kama wanakwenda kunichongea na kwa sababu hii nafasi niliyonayo ninaipenda nisingependa kuipoteza,” amesema.