MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa, Mary Chatanda amesema serikali imepeleka zaidi ya sh. Bilioni moja katika katika kata ya Nyamungusi wilayani Kasulu Mkoani Kigoma
Pia, amewaomba wanawake kuendelea kuunga mkono jitihada za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye amemtua ndoo mama kichwani kwa kupeleka huduma maji hadi majumbani.
Chatanda alisema hayo Kasulu mkoani Kigoma alipotembelea Mradi wa ujenzi wa Mradi wa Maji ambao utahudumia Mitaa 8 wenye wakazi 13,987.
“Serikali ya awamu sita ina lengo kubwa la kuhakikisha inamtua ndoo mama kichwani katika kuwapatia huduma ya maji safi na salama kila kijiji, kitongoji na kata.
“Serikali imeleta zaidi ya shilingi bilioni moja kumaliza tatizo la Maji ndani ya kata yenu hivyo niwaombe wanawake wenzangu kuendelea kuunga mkono jitihada za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye amemtua ndoo mama kichwani kwa kuleta huduma ya Maji hadi majumbani,” alisema.
Mwenyekiti huyo aliipongeza wakala wa Maji na usafi wa mazingira vijijini Ruwasa kuendelea kusimamia kikamilifu Mradi wa Maji ambao umeondoa kabisa changamoto ya Maji katika mji huo.
Hata hivyo, alisema serikali inaendelea kutatua changamoto ya Maji Nchi nzima kwa kuwa wanawake ndiyo wanaopata shida katika maeneo mengi.
“Serikali imemaliza tatizo la Maji maeneo mengi nchini Nawaomba wananchi kuendelea kutunza miundombinu yake kwa kuwa serikali imetoa fedha nyingi na zinawanufaisha nyie wenyewe, hivyo mzingatie hilo,” alisema.
Aliongeza: “Wanawake wa UWT tutaendelea kuzunguka nchi nzima kutangaza na kusemea miradi iliyoletwa na serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambayo imewafikia wananchi wengi.”
Naye, Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Kasulu Mhandisi Edward Kisalu alimpongeza mwenyekiti huyo kwa kutembelea Mradi huo utakaowanufaisha wananchi wengi wa kata hiyo .
“Hivi sasa hakuna changamoto ya Maji katika wilaya Kasulu na wananchi wanapata huduma ya Maji safi na salama maeneo yote,” alisema.