Dereva wa basi la Samwel Coach chupuchupu jela miezi sita

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu dereva wa basi la Samwel Coach, Juma Rajabu kulipa faini ya Sh500,000 au kutumikia kifungo cha miezi sita jela, baada ya kupatikana na hatia ya kumzuia ofisa uhamiaji Daudi Kasanzu kutekeleza majukumu yake.

Hukumu hiyo imetolewa leo Jumanne, Julai 16, 2024 na Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya hukumu.

Hata hivyo, Rajabu amefanikiwa kulipa faini hiyo, hivyo kukwepa adhabu ya kutumikia kifungo cha miezi sita jela.

Hakimu Mwankuga amesema Mahakama imemtia hatiani mshtakiwa baada ya kupitia ushahidi.

“Nimejiridhisha na ushahidi uliotolewa mahakamani hapa dhidi yako na nimejiridhisha kwamba upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha kesi yao bila kuacha,” amesema hakimu Mwankuga.

Amesema mshitakiwa Rajabu ameshitakiwa kwa kosa kumzuia ofisa huyo kutekeleza majukumu yake Juni 28, 2023 katika Stendi ya Magufuli iliyopo Mbezi, jiji Dar es Salaam.

Akipitia ushahidi wa upande wa mashtaka, Hakimu Mwankuga amesema Kasanzu alikuwa akitekeleza majukumu yake katika kituo cha stendi ya Mabasi cha Magufuli na kwamba ushahidi wa Jamhuri ulijenga kesi yao na kusababisha mshitakiwa huyo ajitetee.

“Ushahidi ulio katika rekodi unaonyesha una hatia, hakuna ubishi siku ya tukio ulikuwa kituo hicho cha basi na shahidi watatu alikuja katika basi kwa ajili ya ukaguzi, kwasababu basi hilo lilikuwa likitoka nje ya nchi,” amesema hakimu na kuongeza;

“Pia, haibishaniwi kuwa ofisa huyo wa uhamiaji alipofika baadhi ya abiria walikuwa wameshashuka na kwamba haibishaniwi kulikuwa na malumbano baina yako na ofisa huyo wa ukaguzi na kulazimika kumwita mwenzake kwa usaidizi,” ameongeza.

“Mshakiwa Rajabu, wewe ulitaka ofisa huyo akuonyeshe kitambulisho chake cha kazi, ofisa huyo alikuwa amevaa sare za kazi (uniform), baadhi ya abiria walikuwa wameshuka hivyo hakufanikiwa kufanya kazi inavyopaswa ingawa baadhi yao walirejea,” amefafanua hakimu.

Hakimu amesema maelezo ya onyo yalionyesha kuwa mshtakiwa alikiri kutenda kosa hilo alipohojiwa na hakutoa pingamizi lolote la kisheria, kuyapinga yalipowasilishwa mahakamani kama kielelezo.

Amesema katika kuangalia utetezi wa mshtakiwa, kimsingi anakubali kuwa baada ya tukio la ukaguzi kufanyika, walimtaka aende ofisi ya uhamiaji wakamuelekeze shughuli za kiuhamiaji, lakini alikataa kwasababu maofisa hao hawakumuonyesha kitambulisho.

Mshitakiwa huyo pia, alikubali kwamba mabasi yatokayo nje ya nchi hukaguliwa, hivyo ilikuwa jukumu lake kutii sheria bila shuruti.

Mwankuga amesema, ofisa huyo wa uhamiaji alijeruhiwa siku ya tukio na aliwasilisha nguo alizovaa siku hiyo ambazo zilikuwa na damu.

“Ushahidi huu unaonyesha wazi kwamba kulikuwa na hali ngumu kwa ofisa huyo wa uhamiaji kutekeleza majukumu yake, hivyo ni wazi kwamba mshitakiwa ulitoa ugumu askari huyo kutekeleza majukumu yake na hoja zako kwamba hakukuonyesha kitambulisho hazina mashiko hivyo Mahakama inakuona una hatia kwa kosa uliloshitakiwa nalo,” amesema Mwankuga.

Hakimu baada ya kueleza hayo, Wakili wa Serikali kutoka Idara ya Uhamiaji Mohamed Mlumba ameieleza Mahakama kuwa, hana  kumbukumbu za makosa ya nyuma ya mshitakiwa hata hivyo apewe adhabu kali kwa mujibu wa sheria.

Kabla ya kutolewa adhabu hiyo, Mahakama ilimpa nafasi mshtakiwa kujitetea kwa nini asipewe adhabu kali, hata hivyo Rajabu aliomba Mahakama impunguzie adhabu kwa sababu anategemewa na familia yake, akiwamo baba, mama na ndugu zake anaowasomesha.

Hata hivyo, Mahakama hiyo ilitupilia mbali ombi la mshtakiwa na badala yake ilimhukumu kulipa faini ya Sh500,000 na akishindwa atatumikia kifungo cha miezi sita gerezani.

Related Posts