ELIMU ITAWAOKOA WASICHANA NA UKATILI WA KIJINSIA – WAZIRI DKT. GWAJIMA

Na WMJJWM, Mbeya

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito kwa jamii kuwekeza katika elimu hasa kwa watoto wa kike ili kuwaepusha kufanyiwa ukatili wa kijinsia.

Ameyasema hayo Julai 15, 2024 mkoani Mbeya, katika ziara yake kwenye Chuo cha Maendeleo ya Jamii Uyole yenye lengo la kukagua miradi ya maendeleo.

Akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa hosteli ya wasichana katika chuo hicho, Waziri Dkt. Gwajima amesema kuboreshwa kwa miundombinu chuoni hapo ni kuwawezesha wanafunzi hasa wa kike wanasoma kwa utulivu na kufikia ndoto zao na kuikomboa jamii pia.

“Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameendelea kuboresha miundombinu katika vyuo vyetu 8 vya maendeleo ya jamii. Hosteli hii itagharimu sh. bil.2.8 hadi kukamilika kwake. Wasichana wakielimika, wataweza kujilimda na ukatili wa kijinsia” amesema Waziri Gwajima.

Katika hatua nyingine, Waziri Dkt. Gwajima amewataka wanafunzi wa chuo hicho kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano kupata taarifa muhimu kwa manufaa yao ikiwemo fursa mbalimbali za kiuchumi, wakati akikagua baadhi ya bidhaa zinazotengenezwa na wanachuo kama sehemu ya mafunzo ya kujitegemea.

Kwa upande wake Mkuu wa chuo hicho Sylivester Mwambene amesema hosteli hiyo ya ghorofa tatu itakayochukua wanafunzi 600, itawaondolea changamoto wasichana wanaosoma chuoni hapo kupanga nje ya chuo ambako wanakutana na vishawishi wingi.

Hata hivyo amebainisha kwamba, chuo kina mpango wa kuanza kujenga hosteli ya wavulana pia mara hosteli ya wasichana itakapokamilika.

Related Posts