HAWAJAMALIZA. Hivyo ndivyo unaweza kusema baada ya Yanga kuwa kwenye hatua za mwisho kumalizana na aliyekuwa beki wa kati wa Singida Fountain Gate, Abdulmajid Mangalo ili kuongeza nguvu eneo la ulinzi na kuchukua nafasi ya Gift Fred.
Yanga eneo hilo la beki wa kati linaundwa na nahodha, Bakari Mwamnyeto ambaye ameongezwa mkataba wa kuendelea kubaki hadi 2026, Dickson Job, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ na Gift ambaye inaelezwa kuwa ni miongoni mwa wachezaji ambao wanaachwa kuelekea msimu ujao.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga, kimeliambia Mwanaspoti kuwa, kutokana na Gift kushindwa kupata nafasi ya kucheza mbele ya Bacca, Mwamnyeto na Job, wamefanya uamuzi wa kuzungumza naye wamvunjie mkataba au kumtoa kwa mkopo ili kupisha usajili mwingine mpya.
“Mchakato uliopo ni kumalizana na Gift na kufanya usajili wa beki wa kati wa ndani ambaye ataungana na waliopo kuongeza nguvu eneo hilo ambalo tumeona hakuna sababu ya kuwa na mchezaji wa kigeni ambaye anashindwa kucheza kikosi cha kwanza,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Mbali na hilo, pia kuchelewa kumalizana na Gift kunasababisha kucheleweshwa kwa utambulisho wa Jean Baleke ambaye anaendelea na mazoezi chini ya Kocha Miguel Gamondi, mambo yakienda kama tulivyopanga basi Mangalo na Baleke watatambulishwa muda wowote kuanzia sasa.”
Mwanaspoti lilifanya jitihada za kumtafuta Mangalo kuhusiana na mpango huo ambapo alisema yeye kwa sasa ni mchezaji huru hivyo yupo tayari kuzungumza na timu yoyote huku akikiri kuwa na ofa ya Yanga na moja ya timu kubwa kutoka Kenya ambayo hakutaka kuitaja jina.
“Mimi sio mzungumzaji sana kwani kuna meneja wangu ndiye anashughulikia hayo masuala lakini ameniambia kuna ofa ya Yanga na timu kutoka Kenya ambapo ndio walianza kuhitaji saini yangu ili niweze kuwatumikia msimu ujao, hivyo tunachuja ipi ni ofa kubwa,” alisema na kuongeza;
“Timu ambazo ni nne bora Kenya kuna Gor Mahia, Tusker FC, Polisi Kenya na Bandari, moja kati ya hizi ndiyo zinanihitaji, sitaki kuweka wazi ni ipi kwani ni mchakato ambao umefanyika muda mrefu kimyakimya tofauti na Yanga ambayo wewe umekuja na jina moja kwa moja ndio maana imekuwa rahisi kukuelezea ila mambo yakiwa sawa itajulikana ntacheza wapi.”
Beki huyo alianza kuwa maarufu kwa uchezaji wake akiwa na Biashara United kabla ya kushuka daraja na baadae akatimkia Singida Fountain Gate ambapo pia alifanya vizuri dirisha kubwa kubwa msimu ulioisha alihusishwa na Simba na Yanga lakini mambo hayakwenda sawa akasalia huku hadi sasa alipomaliza mkataba na kutajwa tena timu ya Kariakoo.
Kuelekea msimu ujao, mpaka sasa Yanga imekamilisha usajili wa wachezaji wapya sita ambao ni viungo washambuliaji Clatous Chama na Duke Abuya, mshambuliaji Prince Dube, beki wa kushoto Chadrack Boka, kipa Khumeiny Aboubakar na kiungo mkabaji Aziz Andambwile.