Hukumu kesi ya Ditto dhidi ya DSTV yaahirishwa

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeahirisha hukumu ya kesi ya madai ya mwanamuziki Lameck Ditto dhidi ya Kampuni ya Multchoice Tanzania Limited, maarufu DSTV iliyokuwa itolewe leo Jumanne Julai 16.

Hukumu hiyo sasa itatolewa Julai 22, 2024 mahakamani hapo mbele ya jaji mfawidhi, Salma Maghimbi.

Wakili wa Ditto, Elizabeth Mlemeta ameiambia Mwananchi Digital kwamba hukumu hiyo sasa itatolewa Julai 22.

Ditto ambaye jina lake halisi ni Dotto Bwakeya alifungua kesi ya madai mahakamani hapo mwaka 2020 akiiomba iamuru kampuni Multichoice Tanzania imlipe fidia ya Sh6 bilioni kwa kutumia wimbo  wa Nchi Yangu aliodai ni wake kwenye matangazo yao ya biashara bila ridhaa yake wakati wa kampeni za  fainali ya Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 2019.

Pia, ameiomba Mahakama iamuru alipwe Sh200 milioni kutokana na madhara ya jumla, pia alipwe riba ya asilimia 25 tangu siku alipofungua shauri hilo akidai kampuni hiyo imemnyima fursa ya kunufaika na kazi yake.

Katika kesi hiyo, Ditto alipeleka mashahidi watano na DSTV ilikuwa na mashahidi wawili, Astrid Mapunda na Johnson Mshana wakiongozwa na mawakili, Simon Lyimo na Thomas Mathias.

Upande wa Ditto, baadhi ya mashahidi wake walikuwa ni produzya wa wimbo huo, Emmanuel Maungu (Emma the boy), meneja wa Ditto, Rodney Rugambo na Angela Karashani wakiongozwa na mawikili, Ally Hamza na Elizabeth Mlemeta.

Related Posts