Jonas Mushi: Sitishiki na wachezaji wanaoongoza

WAKATI wachezaji wa timu zinazoshiriki Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) wakichuana kwa ufungaji, lakini  nyota wa JKT, Jonas Mushi ameibuka na kusema hatishwi na hilo.

Mushi amesema ligi hiyo bado ni ndefu, hivyo ana nafasi kubwa ya kuongoza kwa ufungaji katika siku za usoni.

“Tunatakiwa tumalize mzunguko wa pili. Nakuhakikishia nitapambana kuhakikisha narudi katika nafasi yangu niliyoizoea ya kwanza,” alisema Mushi anayecheza nafasi ya shooting guard.

Hadi mzunguko wa kwanza wa mashindano hayo ulipomalizika alikuwa wa saba baada ya kufunga pointi 210, huku nafasi ya kwanza ikishikwa na Amin Mkosa wa Mchenga Stars aliyetupia pointi 268.

Kwa upande wa ufungaji wa maeneo ya mitupo mitatu alishika nafasi ya nane kwa kufunga pointi 27, huku Abdul Kakwaya wa DB Oratory akifunga pointi 42.

Related Posts