Dar es Salaam. Serikali imesema wanasubiri kupangiwa hakimu mwingine ili waendelee na usikilizwaji wa kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kuiba Sh 90milioni, inayowakabili watu watano wakiwamo waliokuwa polisi.
Washtakiwa katika kesi hiyo ya jinai namba 197/2023 ni waliokuwa askari kanzu watatu mwenye namba F 7149 D/Coplo Ramadhani Tarimo (42) maarufu kama Rasta na mkazi wa Kipawa G 7513 D/Coplo Majid Abdallah (35) na mkazi wa Kunduchi na WP 6582 D/ Coplo Stella Mashaka (41) mkazi wa Railway.
Wengine ni waliokuwa wafanyakazi wa Kampuni ya RHG General Traders Ltd ambao ni Ashiraf Sango (31) na Emmanuel Jimmy (31), wote wakazi wa jiji hilo.
Hatua hiyo inatokana na hakimu aliyekuwa anasikiliza shauri hilo Amir Msumi, kuhamishiwa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha na kwenda kuwa Msajili wa Mahakama hiyo.
Wakili wa Serikali, Judith Kyamba ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Julai 16, 2024 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.
“Kesi imekuja kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji, lakini tumeshindwa kumwita shahidi kwa sababu bado haijapangiwa hakimu wa kusikiliza shauri hili, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea,” amedai Kyamba.
Hakimu Msumi baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa mashtaka aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 30, 2024 kwa ajili ya kuendelea na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka linalowakabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.
Itakumbukwa kuwa Julai 2, 2024 Hakimu Msumi aliwaeleza washtakiwa hao kuwa amehamishwa kikazi kutoka Mahakama ya Kisutu kwenda Mahakama Kuu Kanda ya Arusha na huko atakuwa ni Msajili wa Mahakama hiyo.
“Kabla ya kuletwa Mahakama hii (Kisutu) nilikuwa Mahakama ya Mtwara, nimetoka huko nimeletwa Kisutu na sasa natoka Kisutu naenda Mahakama Kuu kanda ya Arusha, kuwa Msajili wa Mahakama hiyo.
“Kwa kawaida unapopokea barua ya uhamisho unakuwa umepoteza mamlaka ya kuendelea kusikiliza kesi, hivyo mamlaka yangu imeishia hapo, baada ya kupewa barua hii ya uhamisho,” amesema Msumi.
Hata hivyo, amefafanua kuwa licha ya kupewa barua ya uhamisho lakini amepewa siku 14 kwa ajili ya kumalizia kusikiliza kesi za mlundikano (Backlog) alizokuwa amepangiwa.
“Nimepewa siku 14 nikabidhi kituo, nimehamishwa kituo changu cha kazi kutoka Kisutu kwenda Mahakama Kuu Arusha, kwa maana hiyo, majalada yote nitayapeleka kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi kwa ajili ya kupangiwa hakimu mwingine,” amesema Hakimu Msumi.
Tayari mashahidi watatu wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao akiwamo, Jones Rugonzibwa ambaye ni Meneja Uendeshaji kutoka Kampuni ya RHG General Traders Ltd, ambaye katika ushahidi wake alieleza namna alivyoshuhudia bosi wake aitwaye Grace Matage alivyolia muda mfupi, baada kuachiwa na askari ambao walikuwa wamemshikilia kwa zaidi ya saa matano eneo la Kurasini, wakishinikiza awapatie fedha.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo, Agosti 28, 2023 eneo la Kurasini, karibu na ofisi za uhamiaji, zililopo Wilaya ya Ilala, siku hiyo ya tukio, washtakiwa kwa pamoja waliiba Sh90 milioni kutoka kwa Grace Donald Matage.
Inadaiwa kabla na baada ya kufanya wizi huo, walimtishia Grace kwa bunduki ili waweze kujipatia fedha hizo bila kikwazo.