Mwanza. Upande wa Jamhuri katika kesi ya kulawiti inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahya Nawanda, umeanza kutoa ushahidi wake.
Kesi hiyo namba 1883/2024, imeanza kusikilizwa leo Jumanne Julai 16, 2024 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Mkoa wa Mwanza, Erick Marley.
Kabla ya kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo, upande wa mashtaka ulimsomea mshtakiwa maelezo ya awali katika kesi hiyo.
Jopo la mawakili watatu wa Serikali likiongozwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Magreth Mwaseba limesoma maelezo hayo kwa kudai mshtakiwa anakabiliwa na kosa la kumlawiti mwanafunzi wa chuo kimojawapo jijini Mwanza mwenye umri wa miaka 21.
Mwaseba amedai mshtakiwa alitenda kosa hilo Juni 2, 2024, katika maegesho ya magari yaliyoko eneo la Rock City Mall wilayani Ilemela, Mkoa wa Mwanza, kinyume na kifungu namba 154 (1) (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16.
Baada ya kusomewa maelezo hayo, Dk Nawanda anayewakilishwa na wakili Constatine Mutalemwa na Alex Ngungulwa amekana kutenda kosa hilo.
Baada ya hatua hiyo, Mwendesha Mashtaka Mwaseba ameieleza Mahakama kuwa upelelezi wake umekamilika na upande wa Jamhuri upo tayari kuanza kutoa ushahidi. Alidai wapo mashahidi wawili kati ya 15 na vielelezo 18 wamewasilisha mahakamani kwa ajili ya kutoa ushahidi wao.
Kutokana na hoja hiyo, Mahakama imeridhia ombi la Jamhuri kuanza kutoa ushahidi, huku mashahidi wakiwa mama mzazi na binti aliyetendewa (aliyelawitiwa) ukitolewa kwa usiri, ili kuhifadhi faragha kama inavyotafsiriwa kwenye kifungu namba 186 (3) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA) marejeo ya mwaka 2022.
Baada ya kuhitimisha ushahidi wao, Mwaseba aliiomba Mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea kutoa ushahidi.
Hakimu Marley alikubali ombi hilo na kusema usikilizwaji wa ushahidi katika shauri hilo utafanyika kwa siku tatu mfululizo kuanzia Agosti 13 hadi 15, 2024 ili kuruhusu haki kutendeka kwa wakati kwa pande zote.
“Kwa kuwa tayari upande wa Jamhuri mmesema mashahidi na vielelezo vyenu viko tayari, Mahakama hii itasikiliza shauri hili mfulululizo kuanzia Agosti 13, mwaka huu,” amesema Hakimu Marley na kuongeza kuwa dhamana ya mshtakiwa inaendelea.
Kesi hiyo iliitwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo, Julai 9, 2024, mbele ya Hakimu Marley, mshtakiwa aliposomewa shtaka alikana.