Marekani kuongeza nguvu mapambano ya saratani nchini

Dar es Salaam. Wizara ya Afya Tanzania na Taasisi ya Biden Cancer Moonshot ya nchini Marekani, wamekaa kikao cha pamoja kutathmini maeneo muhimu ya kushirikiana kupambana na  saratani nchini.

Tanzania na Marekani wamekubaliana kukabiliana na uhaba wa wataalamu, ukosefu wa miundombinu wezeshi, vifaa tiba hasa vya kutoa huduma za mionzi, takwimu, tafiti na ubunifu ili kuwezesha wananchi kupata huduma bora za saratani bila kikwazo.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema hayo leo Jumanne, Julai 16, 2024 katika kikao kilichofanyika Ikulu ya Marekani (White House) Jijini Washington, DC Marekani akiwa ameambatana na Waziri wa Afya wa Zanzibar, Nassoro Mazrui.

Kikao hicho kiliandaliwa na Ikulu ya Marekani kupitia Taasisi ya Biden Cancer Moonshot.

Hatua hiyo inakuja wiki chache tangu ripoti maalumu iliyochapishwa na gazeti hili kuhusu changamoto za huduma za tiba za mionzi, ugunduzi wa mapema na changamoto za gharama za matibabu.

Ripoti hiyo iliyochapishwa kuanzia Juni 24, pia iliangazia upungufu wa vifaa tiba vya saratani ocean road, unavyochelewesha muda wa kupata matibabu ya tiba mionzi kwa wagonjwa na kusababisha vifo vinavyoweza kuepukika.

Katika kikao hicho, Waziri Ummy amesema saratani imekuwa  changamoto kubwa nchini Tanzania na inakadiriwa uwepo wa ongezeko la wagonjwa wapya wa saratani takribani 45,000 kila mwaka.

“Ugonjwa huu wa saratani husababisha vifo 29,743 ambavyo ni sawa na asilimia 66 kwa mwaka, uwepo wa vifo vingi vitokanavyo na ugonjwa huu nchini Tanzania ni kwa sababu wananchi wengi huchelewa kugundulika kuwa na saratani na ukosefu wa huduma za matibabu kwa wananchi,” amesema Waziri Ummy.

Waziri huyo amewashukuru waandaaji wa mkutano huo ambao ni Taasisi ya International Atomic Energy kwa kuamua kushirikiana na nchi za Afrika katika mapambano dhidi ya ugonjwa saratani ili kuokoa maisha ya wengi.

Mratibu kutoka Taasisi ya Biden Cancer Moonshot, Catherine Young wakati akifungua mkutano huo amesema, taasisi hiyo imeandaa kikao hicho muhimu kwa ajili ya kuwaleta pamoja wadau wanaojishughulisha na ugonjwa wa saratani ili kuwezesha Afrika kupambana vyema na ugonjwa huo.

Taasisi hiyo imeahidi kuongeza Dola 10 milioni za Marekani sawa na Sh300 bilioni zitakazosaidia katika mapambano ya ugonjwa wa saratani hususani katika nchi za Afrika.

Mkurugenzi wa masuala ya ukimwi katika ofisi ya Rais, Ikulu ya Marekani Balozi John Nkengasong amesema ni wakati mwafaka sasa kuwekeza katika afua za kinga, mafunzo na utafiti katika magonjwa ya saratani.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya afya kutoka nchi nane za Afrika ikiwamo Tanzania, Sierraleone, Rwanda, BENIN, Zambia, Congo DRC, Lesotho na Msumbiji.

Related Posts