MTOTO WA 12 APONA SELIMUNDU ARUHUSIWA KUTOKA BMH

Na Ludovick Eugene Kazoka, Dodoma

Mtoto wa kumi na mbili (12) kupona ugonjwa wa selimundu baada ya kupandikizwa uloto katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) ameruhusiwa kutoka leo.

Mtoto huyo kwa jina, Caris Anthony, mwenye umri wa miaka 8, amepandikizwa uloto katika Kitengo cha Upandikizaji Uloto BMH tarehe 11/06/2024.

Akiongea na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma, Mama mzazi wa mtoto, Bi Mary Mgumia, ameushukuru uongozi wa Hospitali na Serikali kwa matibabu.

“Namshukuru Rais mama Samia kwa kugharamia matibabu ya mwanangu, Waziri wa Afya, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali Prof Abel Makubi na timu yake kwa huduma hii,” amesema.

Bi Mary anasema mwanae alikuwa anakabiliwa na changamoto ya maumivu ya viungo, akiongeza kuwa hali ilivyozidi kuwa mbaya alimpeleka kituo cha afya.

“Pale kituo cha afya tulifanya vipimo wakatuambia tuende Benjamin (Hospitali ya Benjamin Mkapa) tunaweza tukapata suluhisho,” anasema.

Bi Mary anasema alivyofika BMH, mwaka 2020 vipimo vikaonyesha kuwa mwanae anasumbuliwa na ugonjwa wa selimundu, hivyo mwanae akaanzishiwa dozi pamoja na kutakiwa kuhudhuria Kliniki ya Magonjwa ya Damu.

“Daktari aliyemfanyia vipimo mwanangu aliniambia niondoe wasiwasi kwa kuwa wanatarajia kuanzisha huduma ya upandikizaji uloto ambayo inaponesha kabisa selimundu,” anabainisha.

Dkt William Lloyd, kutoka Kitengo cha Upandikizaji Uloto cha BMH, amesema mtoto atakuwa chini ya uangalizi wa Kliniki ya Magonjwa ya Damu, BMH kwa muda wa mwaka mmoja.

“Nawashukuru wazazi wake kwa kuiamini BMH kwani wangeweza kwenda nje ya nchi kupata huduma hiyo lakini wakaja hapa (BMH),” amesma Dkt Lloyd.

Related Posts