MZEE WA KALIUA: Ahmed Ally ni kama jeshi

KAMA kuna mtu anafanya kazi ngumu kwenye mpira wa sasa hapa nchini ni meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba. Ahmed Ally ndilo jina lake. Wakati mwingine unahitaji kujifyatua akili. Wakati mwingine unaweza kuonekana kama umedata.

Sio kazi rahisi kuisemea Klabu ya Simba hata kidogo. Simba iliyokosa ubingwa kwa msimu wa nne mfululizo. Simba iliyofungwa mabao 5-1 na Yanga. Simba iliyompoteza mfalme wake wa zama hizi, Clatous Chama.

Utawaambia nini watu? Kuna mwamba anaitwa Ahmed Ally hajawahi kukosa cha kuzungumza.

Propaganda na siasa za mpira wetu unahitaji kuwa na mtu kama yeye. Ni burudani ndani ya msiba. Ni mtu anayeweza kukuchekesha wakati machozi yakikutoka. Mmoja kati ya maofisa wa habari mcheshi na mvumilivu.

Kila mtu angetamani kuisemea Simba, lakini sio kwa nyakati hizi ambazo timu imepoteza mwelekeo. Sio kwa nyakati hizi ambazo mashabiki wanalia. Sio kwa nyakati hizi ambazo hakuna wafia timu uwanjani.

Simba imekuwa timu ya kawaida sana misimu minne ya hivi karibuni. Sio tu wamekosa ubingwa, lakini pia timu imekuwa ikicheza vibaya. Pira biriani hakuna tena. Ni mwendo wa kubutua na matokeo mabaya. Ni mwendo wa kufungwa nyingi. Ni mwendo wa kupoteza wachezaji wake wakubwa. Sio rahisi kuisemea klabu yenye mwelekeo huu.

Moja kati ya kazi za maofisa wa habari wa mpira wetu ni kuwaaminisha mashabiki ubora wa wachezaji wao. Kuna muda usipokuwa makini unageuka kuwa kituko. Mashabiki wa mpira wa Tanzania wanapenda sana kusikia wanachotaka kusikia. Wanataka kuambiwa hata wakija Real Madrid kucheza na Simba hawatoki kwa Mkapa. Mashabiki wanataka kusikia Willy Onana anaweza kuanza kwenye kikosi cha kwanza cha Manchester City.

Ndiyo mashabiki wetu. Ndiyo mpira wetu. Kivyetu vyetu. Hapa ndipo unapoona umuhimu wa mtu mama Ahmed Ally kwenye klabu. Mashabiki wetu wanapenda kusikia Joshua Mutale ni kama Jamal Musiala. Mashabiki wetu wanapenda kuambiwa Debora Fernandez hana tofauti yoyote na Jude Bellingham. Huku ndiko mpira wetu ulipo nje ya uwanja. Nasubiri kuona Simba ikitwaa ubingwa na Ahmed Ally. Nasubiri kuiona Simba ikifuzu kucheza fainali kwenye michuano ya CAF.

Bahati mbaya kwa Ahmed ni kuwa tangu ajiunge kama meneja wa Habari na Mawasiliano, Simba haijawahi kuwa Simba. Simba haijawahi kuwa na wakati mzuri chini yake kwenye mashindano makubwa. Muda wote imekuwa timu ya mizengwe. Muda mwingi imekuwa timu ya kusuasua. Anafanya kazi kubwa sana ya kutengeneza hamasa na kispika chake. Kazi kama hizi muda mwingine unalazimika kujizima data ili uweze kufikia malengo.

Hakuna kipindi kilikuwa kigumu kama kwenda kuvaa viatu vya Haji Manara pale Simba. Kwenye mpira wetu, Haji ameongeza sana hadhi ya idara ya habari na mawasiliano. Vijana wengi wa sasa wanapita njia zake. Alifanikiwa sana kuwaaminisha watu mambo magumu. Alifanya kazi nzuri sana kwenye hamasa. Kuondoka kwake kuliacha pengo sio Simba tu, ni kwenye mpira wetu kwa ujumla. Haji ni bingwa wa propaganda. Haji anajua sana siasa za mpira wetu. Isingekuwa rahisi hata kidogo kwa Ahmed kuisemea Simba iliyoachwa na Manara, lakini amefanikiwa.

Ahmed alikubali kwanza kujishusha ili apate pa kuanzia. Alikubali kushuka chini kabisa walipo mashabiki kwa kuwafuata kwenye matawi na kupanda nao mabasi. Ilikuwa akili kubwa sana. Mashabiki wengi wa Simba hasa wale wa chini wanamuona mwenzao.

Bahati mbaya timu imefanya vibaya msimu wa tatu sasa, lakini bado Ahmed yupo nao. Bado hatuna uhakika sana na kitakachotokea msimu unaokuja, labda ni wakati wa Ahmed sasa kujitutumua. Labda ni wakati wa wana Simba sasa kufurahia ubingwa.

Simba wanaonekana kufanya usajili mkubwa, lakini wa wachezaji wengi ambao hawajulikani kwa mashabiki wa soka letu. Washindani wakuu wa ubingwa hapa kwetu ni Simba, Yanga na Azam. Walau pale Yanga watu wanaona majina makubwa yapo. Walau pale Azam unaona sehemu kubwa ya wachezaji mahiri wapo. Simba huoni kitu. Wachezaji wengi watu hawawajui, lakini nadhani ni suala la muda tu.

Miaka ya hivi karibniu baada ya Simba kuteseka, iliamua kwenda kuibomoa Azam FC na kuleta vifaa. John Bocco, Aishi Manula, Shomary Kapombe na Erasto Nyoni na baada ya hapo gari likawaka. Mpira wakati mwingine hauna fomula. Hawa wachezaji wapya wa Simba wanaweza kuja kubadilisha kabisa mwelekeo wa timu. Sio jambo la kuichukulia poa Simba. Wamefanya usajili wa wachezaji wengi wenye umri mdogo na wameonyesha ubora walikotoka. Ni kazi kwa kocha kuunganisha timu. Ni kazi ya wana Simba kuwapa nguvu wachezaji wao. Usiwachukulie poa Simba, wanajua vizuri namna ya kushinda mataji. Usiwachukulie poa Simba kwa sababu humjui mchezaji yeyote waliyemsaini, wanajua wanachofanya.

Hakuna urahisi kwenye kufanikiwa. Mahali ambapo Simba ilikuwa imefikia ilikuwa ni lazima tu wakubali kuanza upya. Timu ilikuwa unga sana. Hata kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ilikuwa ni bahati.

Inaweza kuhitaji muda kidogo huu mpango kazi mpya ili ufanikiwe, lakini wamesajili wachezaji wengi bora na vijana. Kama mazingira ya ligi yetu hayatawasumbua  watakuwa na timu nzuri tu ya kushindana msimu ujao.

Tayari Mzee wa Kispika, Ahmed Ally ameanza kutamba. Kama kawaida yake. Yupo mmoja lakini ni kama jeshi. Amekunywa maji ya bendera nyekundu. Timu ikipepesuka yeye ndiye hugeuka kituko. Sio mtu wa hasıra wala kukata tamaa. Vijana wanaochipukia kwenye uandishi wa habari za michezo na utangazaji wanapaswa sana kumtazama Ahmed kama mtu wa mfano.

Related Posts