Mzee wa miaka 63 auawa Mbozi, anyofolewa viungo vya mwili

Mbozi. Mkazi wa Kijiji cha Nambizo kilichopo Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, Kuminya Sambo (63) ameuawa na watu wasiojulikana huku viungo vya mwili wake ikiwamo miguu na mkono vikiwa vimenyofolewa na mwili kutelekezwa pembeni mwa barabara.

Baadhi ya ndugu wa marehemu pamoja na majirani wamesema mauaji ya mzee huyo aliyekuwa akiishi peke yake, yamewashitua huku wakiliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi na kujua chanzo cha mauaji hayo.

Leo Jumanne Julai 16, 2024, Mwananchi Digital imefika nyumbani kwa marehemu na kuzungumza na mtoto wake, Jose Sambo anayesema baba yake alikutwa ameuawa kandokando ya barabara baada ya kupotea nyumbani kwa takribani siku tatu na wananchi kumtafuta bila mafanikio.

Amesema Sambo alipotea nyumbani usiku wa Julai 9, 2024 hali iliyowafanya wananchi kuungana kumtafuta kwa siku tatu bila mafanikio.

Julai 11, 2024 walimkuta akiwa ameuawa kandokando ya barabara huku mguu mmoja na mkono vikiwa vimenyofolewa.

Grace Sambo, mtoto mwingine wa marehemu amesema baada ya baba yao kupotea, walifika nyumbani kwao na kukuta hakuna dalili zilizoonyesha kama nyumba imevunjwa, lakini walishangaa kuwa amefariki, hivyo wanaliomba polisi kufanya uchunguzi.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Namanga kijijini hapo, Jackson Ntembo baada ya kupewa taarifa za kupotea kwa Sambo walianza kumtafuta na hatimaye kukuta amefariki huku akiwa amekatwa mapanga kifuani, kichwani kisha mguu mmoja na mkono vikiwa vimeondolewa.

“Daktari aliufanyia uchunguzi mwili wa marehemu na kukuta una majeraha manne yaliyosababishwa na kukatwa na kitu chenye ncha kali na mimi kama kiongozi naliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi zaidi juu ya tukio hilo,” amesema Ntembo.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Gallus Hyera amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanaendelea na uchunguzi ikiwa ni pamoja na kuwafuatilia wote waliohusika na mauaji hayo.

Hivi karibuni, Wilaya ya Mbozi imekumbwa na matukio ya mauaji licha ya kwamba baadhi ya waliohusika kwenye mauaji hayo wanashikiliwa na polisi.

Related Posts