Pamba Jiji yachomoa beki Championship 

BEKI wa kulia wa Pamba Jiji, Yunus Lema amesema kucheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza ni ndoto ya muda mrefu iliyotimia, huku akiamini imemfungulia njia ya kufanya vizuri na kucheza soka la kulipwa kimataifa.

Lema amesajiliwa msimu huu na Pamba akitokea Mbuni FC ya Arusha inayoshiriki Championship aliyodumu nayo kwa miaka mitano, huku kiwango chake kikimvutia aliyekuwa Kocha wa Yanga, Nasredinne Nabi katika mchezo wa kirafiki uliopigwa Septemba 30, 2022 na kutaka kumsajili.

Hata hivyo, dili hilo lilikufa kutoka na umri na umbo dogo la beki huyo mmwaga maji, ambapo msimu huu ameibukia Pamba Jiji iliyopanda Ligi Kuu na kutimiza ndoto zake za muda mrefu kucheza katika ligi ya juu nchini.

Akizungumza na Mwanaspoti, Lema amesema mashabiki wa Pamba wasipate mashaka kutokana na umbo lake dogo kwani amejiandaa kukiwasha kwenye Ligi Kuu na kuwadhibiti mawinga wasumbufu wa timu pinzani.

“Ni malengo ya kila mchezaji kucheza Ligi Kuu pia ni moja ya njia zangu kucheza Ligi Kuu, Mbuni ni timu niliyofanya nayo kazi naiheshimu sana imeweza kunipa mwanga kwenye soka na sasa nimeanza safari mpya ya kipaji change,” amesema Lema.

“Watu waje uwanjani kwa wingi na kuangalia soka umri ama umbo langu siyo cha msingi ni kile ninachokitoa kwenye timu, pia kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri.

“Nitafurahi kiukweli kucheza Ligi Kuu ni ligi inayotazamwa na zaidi ya watu milioni 30 ni nafasi ya mimi kuonyesha ulimwengu. Pia malengo yangu ni kucheza soka la kulipwa nje ya mipaka ya bara la Afrika.”

Related Posts