Kigali. Rais mteule wa Rwanda, Paul Kagame amechaguliwa tena kuongoza Taifa hilo huku akiwashukuru wananchi wa Rwanda kwa kumwamini tena kwa kumchagua.
Katika uchaguzi huo uliofanyika Julai 15, 2024, Kagame aliyegombea kupitia chama tawala cha RPF, amepata jumla kura 7,099,810 kati ya kura zote milioni 9,071,157, ushindi huo ni sawa na asilimia 99.15.
Amefuatiwa na Frank Habineza, mgombea wa chama cha Democratic Green aliyepata jumla ya kura 38,301 sawa na asilimia 0.53 na Phillipe Mpayimana aliyepata kura 22,753 sawa na asilimia 0.32.
Unaweza kusema matokeo ya wagombea hawa yanajirudia kama ilivyoshuhudiwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 wakati Kagame aliposhinda uchaguzi huo kwa kuwaacha mbali wapinzani wake kwa kupata asilimia 99 ya kura zote zilizopigwa.
Kagame mwenye umri wa miaka 66, sasa ataiongoza Rwanda kwa miaka mitano katika awamu yake hii ya nne badala ya saba kama ilivyokuwa katika awamu tatu zilizopita.
Hiyo ni kutokana na kufanyika kwa mabadiliko ya Katiba ya nchi hiyo, mwaka 2017, yaliyoeleza kuwa Rais atakayechaguliwa kushika madaraka, ataiongoza Rwanda kwa kipindi cha miaka mitano badala ya saba kama ilivyokuwa awali.
Akizungumza kwa mara ya kwanza baada ya matokeo hayo, Kagame amewashukuru Wanyarwanda kwa kumwamini tena na kumchagua kuliongoza Taifa hilo kwa muhula mwingine na kwamba imani hiyo inampa nguvu zaidi ya kujiamini.
Amebainisha kwamba mchakato wa uchaguzi, kampeni walizofanya, upigaji kura na matokeo ambayo yametangazwa, yanamaanisha kitu muhimu katika maisha ya mtu na inaashiria uaminifu, ambao ninakushukuru.
“Uaminifu si rahisi kupatikana; hakuna kitu unaweza kumpa mtu ili kupata imani yake ya haraka. Uaminifu hujengwa kwa muda mrefu. Kwa uaminifu huu na miaka hii yote tumekuwa pamoja katika kutatua changamoto nyingi ngumu, kuna wakati uliniona nimeshindwa kupata suluhisho?
“Sijawahi kushindwa na changamoto. Hata katika hali ngumu tuliyopitia au tutakayopitia siku za usoni, uaminifu ndio sababu ya yote. Uaminifu wenu inanifanya nijiamini, hakuna changamoto ambayo hatutashinda,”
Katika chaguzi zilizopita, Kagame alishinda kwa zaidi ya asilimia 93 ya kura mwaka 2003, 2010 na 2017 alipata asilimia 98.79 katika uchaguzi wa hivi karibuni, ikilinganishwa na asilimia 0.48 tu ya Habineza na asilimia 0.73 ya Mpayimana.
Rais Kagame amekuwa akitawala siasa za Rwanda tangu majeshi ya waasi yachukue mamlaka mwishoni mwa mauaji ya kimbari yaliyofanyika mwaka 1994 huku Watutsi 800,000 na Wahutu wenye msimamo wa wastani wakiuawa.
Tangu wakati huo, wananchi wengi wa nchi hiyo wamekuwa wakimsifu kiongozi huyo kwa uimara wake katika kuimarisha uchumi na kuleta maendeleo. Amefanikiwa kusimamia kwa nguvu ujenzi wa miundombinu mbalimbali na kuanzisha miradi mingi ambayo imesaidia Rwanda kuongoza katika eneo la Afrika Mashariki, ikilinganishwa na nchi nyingine.
Wakizungumza baada ya kupiga kura Jumatatu Julai 15, 2024, baadhi ya wananchi waliojitokeza wamesema waliamini kuwa kiongozi huyo atashinda kwa kuwa ana uwezo wa kuifanyia makubwa nchi yao.
Janeth Ndahinda, mkazi wa Kigali, amesema: “mimi nilikuwa naamini kwamba Kagame anashinda tena huu uchaguzi, kwa haya tunayoyaona, sijui kama kuna mtu ataweza kumtoa hivi karibuni, bado.”
Ndahinda amesema ili mgombea awe na mtaji wa kura, ni lazima awawezeshe vijana ili waje wamsaidie baadaye, amedai kwamba hicho ndicho anachokifanya Kagame hivi sasa.
“Anajaribu sana kuwaimarisha vijana na wanawake huko vijijini, anatupatia matibabu, vurugu hakuna tena, huyu ni baba wa Taifa letu na leo anashinda kama mwaka 2017 kwa kura nyingi,” amesema Ndahinda.
Akiwa na mtazamo tofauti, mkazi wa Kigali, Roberty Ulyakozi amesema licha ya kuwa Kagame ameyafanya mengi mazuri, anapaswa kukumbuka kuwa uongozi ni kupokezana kijiti.
“Ameongoza kwa muda mrefu, amewapigania Wanyarwanda, tunamshukuru, lakini muda wake umefika mwisho awaachie na wengine. RPF ina watu wengi wenye uwezo wa kuongoza kama yeye, sasa inatosha, najua nimepiga kura na atashinda tu lakini atumie busara tu ya kuachiana madaraka,” amesema bila kufafanua kwa nini anataka Kagame aondoke madarakani.
Wakosoaji wengine mambo wanaodai kuwa Rais Kagame amekuwa akiuminya upinzani, ndiyo maana anashinda mara zote kwa kishindo kwa kile wanachodai kuwa wapinzani wenye nguvu hawapewi nafasi nchini humo.
Jacton Mutoni amesema penye moshi daima huwa panafuka moto: “Hatukatai Kagame katufanyia mambo makubwa sana na hakuna Mnyarwanda mwenyewe anaweza kubisha, lakini anatukera jambo moja tu la kuminya upinzani, mfano safari hii Tume ya Uchaguzi imewakata hata wagombea huru waliojitokeza kwenye nafasi za ubunge, sasa hapa utasema kuna upinzani?” amehoji Mutoni.
Hata hivyo, itakumbukwa Julai 13, 2024 alipokuwa akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari baada ya kuhitimisha kampeni zake, Kagame alisema kwa mara ya kwanza kwamba nafasi ya urais aliipata kama ajali tu, hakutarajia kama angeweza kuiongoza Rwanda akiwa Rais.
Hivyo, aliwataka wote wanaouliza maswali kuhusu mrithi wake, waliache suala hilo mikononi mwa Wanyarwanda wenyewe.