USHINDI wa JKT Stars dhidi ya Polisi Stars wa pointi 98-82 katika Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), ulichangiwa na pointi 23-13 ilizopata katika robo ya tatu.
Mchezo huo uliokuwa mkali na wa kusisimua uliofanyika katika Uwanja wa Donbosco Youth Centre, Upanga.
Katika mchezo huo JKT Stars iliongoza katika robo ya kwanza kwa pointi 21-16, 24-32 hadi kufikia mapumziko na Polisi Stars walikuwa mbele kwa pointi 48-45.
Robo ya tatu ilipoanza Polisi walionekana kuchoka na JKT Stars ikatumia udhaifu huo kupata pointi 23-13 na robo ya nne ikapata pointi 20-21.
Katika mchezo huo, Jesca Julius aliongoza kwa kufunga pointi 18 akifuatiwa na mchezaji mwenzake Sara Budodi aliyefunga pointi 12.
Upande wa Polisi Stars aliyeongoza katika ufungaji ni Irene Kapambala aliyefunga pointi 16 akifuatiwa na Winfrida Chikawa na Mkerenge Hassan waliofunga pointi 13 na 14 mtawalia.
Katika mchezo mwingine uliocheza uwanjani hapo, JKT iliishinda Mgulani kwa pointi 76-56.