Serikali yapokea dozi chanjo ya ugonjwa wa Sokota

Arusha. Serikali imepokea dozi milioni 3.9 ya chanjo ya ugonjwa wa Sotoka kwa ajili ya mbuzi na kondoo kutoka Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa mataifa (FAO).

Akipokea chanjo hiyo mkoani Arusha leo Jumanne Julai 16, 2024 baada ya kufungua kongamano linalohusisha sekta ya umma na sekta binafsi kuhusu ushirikiano katika utoaji wa huduma za afya ya mifugo.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Riziki Shemdoe amesema , chanjo hiyo itasaidia kuchanja wanyama hao kwa ajili ya kuzuia magonjwa ya Sotoka.

Ugonjwa wa Sotoka ni ugonjwa ambao  unaathiri maeneo kadhaa  ya mbuzi na kondoo ikiwemo  mfumo wa upumuaji kwa sababu mifugo hupata vidonda mdomoni, makamasi puani, na kuwakosesha hamu ya kula na kusababisha  kudhoofu.

Profesa Shemdoe amesema bado mahitaji ya chanjo nchini ni makubwa na kuomba wadau mbalimbali kuendelea kusaidia katika kutoa chanjo hizo ili kuweza kufikia malengo yaliyowekwa.

“Kwa mwaka huu wa fedha 2024/2025 serikali imetenga kiasi cha Sh28 bilioni kwa ajili ya kampeni ya utoaji wa chanjo za mifugo nchi nzima ambapo  kampeni hizo zinatarajiwa kuanza mwaka huu wa fedha na itasaidia sana kumaliza magonjwa hayo ya mifugo nchi nzima,”amesema Profesa Shemdoe

Profesa Shemdoe ameongeza lengo la kongamano hilo la wataalamu wa mifugo kutoka Tanzania na nje ya nchi ni kuangalia masuala muhimu ya afya ya mifugo kwani wamekuwa wakifanya hivyo mara kwa mara katika kuwafundisha wataalamu hao hivyo wameweza kukutana ili kuweka mikakati ya pamoja namna ya kuboresha sekta hiyo.

“Lengo la wizara ni kuhakikisha tunatoka kwenye asilimia 7 hadi 8 ya pato linatokanalo na Mifugo na kuweza kufikia asilimia 10 ndani ya miaka miwili hadi mitatu na kwenda mbele zaidi kwani hayo ndo malengo ya wizara kuhakikisha tunasonga  mbele huku tukishirikiana na taasisi binafsi pamoja na mashirika mengine na wadau mbalimbali  “amesema Shemdoe

Mwakilishi wa FAO, Stella Kiambi amesema wametoa chanjo hiyo kwa Serikali kwa ajili ya uchanjaji wa mifugo  nchini Tanzania  na wataendelea  kuangalia namna ya kusaidia zaidi katika kuhakikisha wanaunga mkono Serikali katika kutoa msaada zaidi ili kuwa na wanyama wenye afya njema.

Kwa upande wake Mkurugenzi kutoka Shirika la afya ya wanyama ulimwenguni (WOAH) kwa upande wa Afrika Mashariki, Dk Samuel Wakhusama amesema wamekuwa wakisaidia nchi nyingi ziwe na uhakika  wa afya ya wanyama na kuhakikisha  hakuna madhara ya wanyama.

Naye Mwenyekiti wa sekta binafsi -Veterinary, Alex Chang’a amesema wamekuwa wakishauri wafugaji kuwa na mazao bora ya mifugo kwa kuwapatia chakula kizuri na kuwa na afya bora.

Related Posts