Serikali yasisitiza wananchi wajengewe uwezo kuhimili nishati safi ya kupikia

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis amezitaka taasisi mbalimbali kutengeneza mazingira yatakayowezesha wananchi kuhimili matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuiokoa Tanzania na uharibifu wa mazingira.

Ripoti ya mwaka jana iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) inaonyesha watu bilioni 2.4 duniani wanategemea nishati chafu ya kupikia hali inayosababisha hekta milioni 3.9 za misitu kupotea kila mwaka katika Bara la Afrika.

Akizungumza Julai 14,2024 wakati wa tamasha la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia lililoandaliwa kwa ushirikiano wa Taasisi ya Upskills, amehimiza matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuongeza juhudi za upandaji miti kwa wingi kunusuru mazingira.

“Bado tunaendelea kupata athari za uharibifu wa mazingira ambazo kubwa ni ukataji miti ovyo kwa shughuli za mifugo, kilimo na nyingine. Katika kampeni za upandaji miti tunataka hata wanafunzi, walimu wote waelekeze nguvu kwenye kampeni ya Mama Samia ya upandaji miti ili Tanzania iwe ya kijani.

“Badala ya kukata keki kusherehekea siku ya kuzaliwa tupande miti kunusuru taifa dhidi ya uharibifu wa mazingira, watu wakioana au kuachana pandeni mti…Ilani ya Uchaguzi kifungu cha 235 inaelekeza kila halmashauri ipande miti milioni 1.5 kutunza na kuhifadhi mazingira,” amesema Khamis.

Naibu Waziri huyo pia amewataka wamiliki wa viwanda, migodi, mifugo kuepuka kuchafua vyanzo vya maji na kutengeneza mifumo mizuri ya kunusuru maji machafu yasiingie kwenye vyanzo vya maji.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Upskills, Tinna Masaburi, amesema waliandaa tamasha hilo kwa lengo la kuelimisha umma kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kutunza mazingira na kupunguza ukataji miti ovyo hasa katika Jiji la Dar es Salaam ambalo ndilo linafanya biashara kubwa ya kuni na mkaa.

“Serikali iongeze nguvu kuhakikisha mkaa mbadala unapatikana kwa wingi na kwa bei nafuu ambazo wananchi watazimudu, Watanzania watumie nishati safi ya kupikia kuinusuru nchi kutokana na ukataji miti na uharibifu wa mazingira,” amesema Tinna.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Dar es Salaam, Janeth Masaburi, amesema wanatambua jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo ameweka lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya wanawake wanatumia nishati hiyo ifikapo mwaka 2030.

Katika tamasha hilo Taasisi ya Upskills ilimtunuku tuzo ya heshima Rais Samia Suluhu Hassan kutambua jitihada zake za kuhamasisha jamii kutumia nishati safi ya kupikia.

Related Posts