Nairobi. Shirika la Ford Foundation la Marekani linalofanya kazi zake nchini Kenya limekanusha tuhuma za Rais William Ruto kuwa wanahusika kufadhili maandamano ya Gen Z.
Taarifa rasmi iliyotolewa leo Jumanne Julai 16, 2024 na Mkurugenzi wa mawasiliano wa shirika hilo, Tolu Onafowokan inasema hawahusiki na maandamano yao, pia sera yao haiwafungamanishi na upande wowote.
“Hatujafadhili maandamano ya hivi karibuni yanayopinga muswada wa sheria ya fedha, tuna sera isiyoegemea upande wowote katika utoaji wa ruzuku,” amesema Onofowokan.
Aidha, katika taarifa hiyo Ford inaeleza kuwa, wanatambua haki ya Wakenya kutetea amani na haki bila vurugu au ghasia.
“Tunatambua haki ya Wakenya kutetea nchi yao kwa ajili ya amani, haki na usawa, tunakataa vitendo au matamshi yoyote ya chuki au kuleta ghasia dhidi ya taasisi yoyote, mtu binafsi au jamii,” inaeleza taarifa hiyo ya Ford Foundation.
Rais Ruto jana Julai 15, 2024 akihutubia Nakuru alilishutumu Shirika la Ford Foundation kudhamini maandamano ya Gen Z yaliyotokea mwezi uliopita nchini humo.
“Nataka niulize watu wa Ford Foundation watuambie hiyo pesa wanatoa, wanatoa ifanye fujo ndio wapate faida gani? Tutawaita na tutawaambia kama hawapendi demokrasia nchini Kenya, kama watafadhili vurugu na machafuko tutawaita na tutawaambia wao pia kujirekebisha au waondoke,”amesema Rais Ruto.