SHULE ZILIZOFANYA VIBAYA ZAPOKEA ZAWADI YA VINYAGO – MWANAHARAKATI MZALENDO

 

Serikali Wilayani Bunda imewaagiza watendaji wa kata na vijiji kusimamia suala la lishe mashuleni ili kusaidia kuinua kiwango cha ufaulu kwa watoto.

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dkt. Vicent Anney ametoa agizo hilo wakati akikabidhi ngao na vinyago kwa shule zilizofanya vizuri na vibaya mtawalia katika mtihani wa kidato cha nne mwaka 2023.

Katika zoezi hilo baadhi ya walimu ambao shule zao zimefanya vibaya walidai kuwa utoro na ukosefu wa lishe kwa shule hizo vimechangia wanafunzi kufanya vibaya katika masomo na mitihani.

Kufuatia hali hiyo, Serikali imeelekeza kuanzisha huduma ya lishe katika shule hizo na kuwataka watendaji wa vijiji na kata kuhakikisha wanasimamia suala hilo la lishe.

Shule zilizofanya vizuri wilayani humo na kupokea ngao ya ubora ni Shule ya Sekondari Ikizu na Bunda Day huku zilizoshika mkia na kupokea vinyago zikiwa ni Hunyari Sekondari na Wariku.

Utoaji wa ngao na vinyago hivyo ni utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi alilolitoa hivi karibuni kwa kuzitaka shule zilizofanya vizuri kupongezwa kwa ngao na zilizofanya vibaya kupewa kinyago ikiwa ni sehemu ya kuzihamasisha kufanya vizuri kwa mwaka mwingine.

 

Chanzo : TBC Online

Related Posts